ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo ambayo ameifanya katika Mkoa wa Dodoma imeanza kuzaa matunda baada ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeamua kubadilisha kanuni zake kuanzia msimu ujao wa kilimo.
Kanuni ambazo zimebadilishwa zinahusu vifungashio vya mbolea ambapo vitakuwa katika ujazo wa kuanzia kilo moja na kuendelea tofauti na zamani ambapo ujazo wa mbolea za kilimo ilikuwa ni kuanzia kilo 25 na kuendelea.
Uamuzi wa Wizara ya Kilimo kuamua kubadili kanuni hizo umetokana na kilio cha wananchi ambao walimueleza Katibu Mkuu akiwa katika ziara yake kwenye wilaya mbalimbali za mkoa huo.Hivyo leo wakati anahitimisha ziara yake Serikali imetoa maelezo ya kubadilisha kanuni hizo.
Akizungumza mbele ya wananchi Waziri Hussein Bashe aliamua kutangaza utaratibu mpya ambao utawezesha wakulima kununua mbolea kwenye ujazo wa kuanzia kilo moja na kuendelea.
Kabla ya Waziri Bashe , Katibu Mkuu Chongolo alimtaka Waziri huyo kutoa kauli kuhusu ujazo wa mbolea kwani ni miongoni mwa malalamiko aliyoyapokea kutoka wananchi.