Sehemu kubwa ya umati wa wanachama, wakereketwa, wapenzi na wananchi wa Dodoma Mjini wamehudhuria mkutano wa hadhara leo Juni 25, 2023 katika viwanja vya Central Sekondari ambapo Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Daniel Chongolo amezungumza na wananchi ikiwa ni uhitimishaji wa ziara yake ya siku 10 mkoani Dodoma.
Ndugu Chongolo leo anahitimisha ziara yake ya siku 10 aliyoianza katika mkoa wa dodoma ambapo aliambatana na katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndg. Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndg.Issa Gavu.
Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia uhai wa Chama hicho pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma.
Katibu Mkuu alianza ziara yake katika mkoa wa Dodoma Juni 15 , 2023 na amepita katika Wilaya za Mpwapwa, Kondoa, Chemba, Bahi, Kongwa na Chamwino ambapo mbali ya kukagua utekelezaji wa Ilani amepata nafasi ya kusikiliza changamoto za wananchi.
Changamoto hizo zilikuwa zinatolewa na wananchi katika mikutano ya hadhara na vikao vya Chama vilivyokuwa vinafanyika katika ngazi ya Shina ,na miongoni mwa changamoto alizopokea ni ucheleweshaji wa ulipaji fidia kwa wananchi walioathiriwa na tembo.
Pia katika ziara hiyo Chongolo amesikiliza malalamiko ya kuchelewa kwa kutekelezwa kwa miradi ya skimu za kilimo cha umwagialiji na akiwa Wilaya ya Kondoa alipokea kilio cha uhaba wa chakula hasa jimbo la Kondoa Vijijini kiasi cha kumuomba Katibu Mkuu huyo kufikisha ombi lao kwa Serikali ione uwezekano wa kuwapatia chakula.
Mengine ambayo Chongolo ameyapokea kama changamoto za wananchi ni changamoto ya uhaba wa maji, migogoro ya ardhi , afya na miundombinu.
Hata hivyo, uhitimishaji wa ziara yake Katibu Mkuu amekuwa na utamaduni wa kufanya majumuisho yanayokwenda sambamba na kutoa maelekezo kwa watendaji na viongozi wa ngazi mbalimbali, lengo likiwa kuona changamoto zote zipatiwa ufumbuzi ambapo leo majumuisho ya ziara hiyo yamefanyika Jijini Dodoma.