Mavunde kutoa milioni 20 kila mwaka kuanzisha viwanda vidogo.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameanzisha Tuzo maalum ya Wajasiriamali ambayo italenga katika kuongeza wigo wa uchakataji bidhaa za kilimo na mifugo kwa kukipatia mitambo na mashine ndogo zenye thamani ya Tsh 20,000,000 kikundi kimoja kitakachopitishwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO)kila mwaka.

Mavunde ameyasema hayo jana katika Viwanja vya Nyerere Square wakati akifunga mafunzo ya wajasiriamali mkoani Dodoma chini ya mwavuli wa Taasisi ya Wanawake na Uchumi wa Viwanda (WAUVI).

“Ninawapongeza sana WAUVI kwa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali wa Dodoma ili kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha.

Ninaona jitihada kubwa sana za Wajasiriamali hapa Jijini Dodoma ambao naamini tukiwasaidia kwa kuwaongezea mtaji na mashine za kisasa wanaweza kupiga hatua na kuleta mapinduzi makubwa.

Tunamshukuru Mh Rais Dr. Samia S. Hassan kwa kuendelea kutengeneza fursa nyingi zaidi za kiuchumi kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea wa kuijenga Makao Makuu Dodoma.

Mimi kwa nafasi yangu nitahakikisha tunawasaidia wajasiriamali ambao wameshapiga hatua na kuhitaji mitambo na mashine ndogo kukua zaidi kiuchumi.

Nitaanzisha tuzo ya Mavunde ya Wajasiriamali ambayo lengo lake kubwa litakuwa ni kupata kikundi cha kuongeza thamani ya mazao na mifugo ambacho tutakipa mitambo na mashine ya Tsh 20,000,000 na kukilea mpaka kukua kwake” Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Mwenyekiti wa Wauvi Taifa Bi. Rehema Mbeleke amesema mafunzo hayo kwa wajasiriamali 3000 yana lengo ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wa Dodoma ili kushiriki katika masoko ya ushindani wa bidhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *