Makamba awaomba Watanzania kuwapa muda na subira kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Wizara ya Nishati ni Wizara inayosimamia sehemu kubwa ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini kwasasa ambayo inayohitaji umakini katika kuitekeleza na hivyo kuwaomba wananchi kuwapa muda na subira katika kutekeleza miradi hiyo.

Waziri Makamba ameyasema hayo wakati anazungumza mtandaoni katika mtandao wa ClubHouse mwishoni mwa wiki hii na kusema majukumu waliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni makubwa sana na wako kazini kwa kasi kubwa kila siku kuyatekeleza.

“Tunashukuru Rais Samia ametuamini katika dhamana hii ya nishati ambayo ni kubwa sana. Katika miradi mikubwa ya kimkakati iliyoainishwa na Serikali, sisi (Wizara ya Nishati) takribani nusu ya miradi yote ya kimkakati ni miradi ya nishati. Kwahiyo tunayo kazi kubwa sana kuhakikisha miradi hii yote inakwenda vizuri na inatimiza malengo yake.” Alisema Makamba.

“Tunachoomba sisi ni muda na subira, kwasababu kazi hizi matokeo yake yanachukua muda na hukumu ya kazi tunayoifanya tungeomba itolewe mbele na sio sasa. Sisi Wizarani tuko makini sana na taasisi zetu zote kuanzia TPDC, TANESCO, REA na EWURA ziko makini sana na hata utamaduni wa kufanya kazi umebadilika sana na kumekuwa na mashirikiano na kusaidiana sana ili kufikia malengo ya Taifa kwa miradi yote mikubwa tunayotekeleza.” Aliendelea kusema Waziri Makamba.

Waziri Makamba amesema Wizara hiyo kwasasa iko kwenye mageuzi makubwa sana ya kupika miradi mikubwa ya kimkakati itakayokuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa huku akisema Wizara hiyo ina changamoto nyingi ikiwemo za rushwa, mikataba mibaya, masuala ya zabuni na kadhalika lakini wanahakikisha masuala yote yanafanyika katika misingi ya uadilifu.

Wizara ya Nishati pamoja na miradi mingine mikubwa kama ile ya kusafirisha umeme kwenye gridi ya Taifa, kupeleka umeme Vijijini kupitia REA, gesi asilia (LNG) na mingine mikubwa, kwasasa Wizara hiyo inatekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme kwa njia ya maji wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere kule kwenye Mto Rufiji ambao utazalisha takribani Megawatts 2,115 kwa mpigo pindi utakapokamilika na kuondoa uhaba wa umeme nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *