Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo amesema Serikali ya awamu ya sita imekuwa sikivu kwa kutatua changamoto za wananchi kwa kasi kubwa na wakati wote .
Chongolo amesema hayo leo Mei 27,2023 muda mfupi baada ya kushiriki ujenzi katika shule ya msingi Muungano iliyopo kata ya Boma mafinga katika wilaya ya Mafinga ,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 7 ya kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya ccm 2020-2023.
Amesema shilingi Milioni 347.5 zilizopelekwa katika shule ya Muungano kujenga madarasa ni ushahidi tosha kuonesha namna Serikali ya CCM inavyojali wananchi wake.
Chongolo amewataka wakazi wa eneo hilo kutosikiliza maneno ya wanasiasa waongo ambao wamekuwa wakiwagombanisha na Serikali yao ambayo imekua ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
Amewataka wazazi kuwasimamia watoto katika suala zima la elimu kwa kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya elimu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita
Awali mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendegu amesema ujenzi wa shule hiyo ya Muungano inatokana na shule ya awali kujaa wanafunzi na hivyo Serikali ikaona ni vema kuanzisha ujenzi mpya wa madarasa katika shule ya Muungano.