
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewakata Watanzania wasishawishike kuivuruga amani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Amesema wanaoshawishi kuivuruga amani, familia zao zina makazi nje ya Tanzania, hivyo wanafanya hivyo kwa sababu wanapo pa kukimbilia.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Oktoba 1, 2025 alipozungumza na wananchi wa Hai, mkoani Kilimanjaro, katika mkutano wake wa kampeni za urais, zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Amesema wananchi wasikubali kushawishiwa, kwani kufanya hivyo kutasababisha waharibu amani ya nchi.
“Msikubali kushawishiwa tukaharibu amani ya Tanzania. Msikubali hata kidogo. Wanaoshawishi wanapo pa kwenda.
“Familia zao haziko hapa. Wapo wao kuja kufanya fujo, kukikorogeka wakimbie wakaungane na familia. Sisi tunakwenda wapi? Ni hapa hapa Tanzania,” amesema Dkt Samia.

