Bil. 22/- za mradi wa TACTIC kunufaisha wananchi wa Manispaa ya Moshi

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

JUMLA Sh. bilioni 22.9 zinatarajiwa kunufaisha wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Moshi Mkoani Kilimanjaro katika Utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania maarufu kama TACTIC.

Moshi imeingia katika kundi la pili, la mradi utakaotekelezwa na Mkandarasi mzawa M/s Hari Singh and Sons Limited in Joint Venture na Peritus Exim Private Limited kwa kipindi cha miezi 15 kuanzia Oktoba Mosi, 2025.

Wakati wa utiaji saini Mkataba wa Ujenzi huo leo Jumamosi Septemba 27, 2025 Mjini Moshi, akiongea kwa niaba ya mtendaji mkuu wa TARURA Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, Mhandisi Emmanuel Manyanga amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, mitaro ya maji ya mvua pamoja na ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi.

“Kazi za ujenzi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Ruwaichi- Njoro (Km 6.9), Barabara ya pepsi ya Km 1.25, Ujenzi wa barabara ya Shirimatunda- Magereza (Km 5.1), Mtaro wa Ushirika- Keys hotel- Moshi Pazuri (Km 2.0), ujenzi wa Mtaro wa Kibong’oto (Km 1.9) pamoja na jengo la ghorofa mbili la usimamizi na uratibu wa mradi,” amesema mhandisi Manyanga.

Kulingana na mhandisi Manyanga, pamoja na uboreshaji wa miundombinu amesema mradi huo wa TACTIC utahusisha pia kuzijengea uwezo Taasisi zote za Wizara,TARURA pamoja na Halmashauri ya Miji kupitia mafunzo mbalimbali yenye kulenga kuboresha utendaji kazi, ufanisi wa huduma mbalimbali kwa jamii pamoja na kununua vitendea kazi kama vile magari ya usimamamizi na ufuatiliaji pamoja na kuhuisha mifumo ya ukusanyaji mapato.

Mradi wa TACTIC ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya dunia wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 410, malengo yakiwa ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ta Tanzania pamoja na kujenga uwezo wa Halmashauri ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji miji. Mradi huo unajenga miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara kulingana na vipaumbele vya Halmashauri, kuimarisha usimamizi wa uendelezaji Miji pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa wananchi na Halmashauri husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *