
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
PAMOJA na dhamira yake ya kukuza uchumi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake pia, itahakikisha inajenga kizazi kijacho chenye maadili kwa maslahi ya Taifa.
Utekelezwaji wa hilo, kwa mujibu wa Dkt. Samia, utafanyika kwa kuhakikisha teknolojia itakayofundishwa shuleni na kutumika inalinda mila, desturi na tamaduni za nchi, zipewe hadhi ili vijana wazifuate, badala ya kuiga za nje.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo Mjini Mtwara jana, alipozungumza na wananchi wa mkoa huo, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais, zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Akiijenga hoja hiyo, Dkt Samia amesema dhamira yake katika miaka mitano ijayo ni kupiga hatua kubwa za matumizi ya teknolojia wakati huo huo, hatua za makusudi zikichukuliwa kudumisha, mila, desturi na tamaduni.
“Miaka mitano ijayo itakuwa miaka ya kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia za kisasa na vile vile miaka mitano ijayo tunataka kuchukua hatua za makusudi kudumisha mila na desturi zetu zile zilizo bora,” amesema.
Katika kufanikisha hilo, alisema teknolojia itakayofundishwa itaunganishwa na mila, desturi na tamaduni za Tanzania ili isifute, kuharibu, au kuwapotosha vijana wakakiuka mila na desturi.
“Kwa kadri inavyowezekana teknolojia tunayokwenda kuitumia tunataka ikalinde mila, desturi na tamaduni zetu na tuzirithishe kwa vijana wetu badala ya kuona tamaduni za nje na wakazifuata, wafuate hizi za kwetu, tuzipe hadhi wazifuate hizi za kwetu,” amesema.
Dkt Samia alisema malengo yake ni kuhakikisha kinajengwa kizazi zijacho chenye maadili ili kuondoa ombwe la maadili linalolalamikiwa na viongozi wa dini kwa sasa.
Matumizi mengine ya teknolojia itakayofundishwa, alisema ni katika sekta ya kilimo kuhakikisha wakulima wanalima kwa nyenzo bora na wanazalisha zaidi.
Ameeleza hata zana za kilimo zitakazotumika zitakuwa za kisasa na kutakuwa na mpango wa wakulima kukodishiwa zana kwa bei nafuu ili wazitumie kisha zinarudishwa vituoni.

Uzalishaji korosho
Katika hatua nyingine, Dkt Samia amesema Tanzania imeshika nafasi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa korosho, nyuma ya Ivory Coast.
“Nchi yetu Tanzania ni ya pili kwa Afrika katika kuzalisha korosho, wanaotupita ni nchi inaitwa Ivory Coast wa pili ni sisi. Kwa hiyo tutaendelea kuweka jitihada ili twende sambamba na nchi hiyo ambayo sasa inaongoza,” amesema.
Hatua hiyo, amesema imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo, kulikosababishwa na uamuzi wa Serikali kutoa ruzuku ya pembejeo katika zao la korosho.
Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake pekee, amesema Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo yenye gharama ya Sh. bilioni 726 kwa ajili ya kugawa mbolea za ruzuku nchini kote.
“Kila mwaka tunatumia kiasi cha Sh152 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo, fedha ambayo ingetoka mfukoni kwa wakulima. Lakini tumeibakisha mifukoni mwao Serikali tunagawa kwa ruzuku nusu bei, lakini vitu vingine bure,” amesema.
Amesema Serikali yake inafanya hivyo kwa sababu amedhamiria kukuza kilimo na uzalishaji wa korosho.
Amesema hatua hiyo imesababisha uzalishaji wa korosho ukue kutoka tani 118,811 mwaka 2020/21 zilizouzwa kwa thamani ya Sh265 bilioni hadi tani 330,505 mwaka 2025 zilizouzwa kwa Sh1.9 trilioni.
“Haya ni manufaa makubwa sana kwa wakulima, isingekuwa ruzuku basi uzalishaji ungeshuka na mapato kwa wakulima ungeshuka kwa sababu tungezalisha vile vile tu, nikiweza nanunua dawa napuliza nikishindwa basi tu, kwa hiyo tutaendelea na huduma hizo ili kukuza uzalishaji,” amesema.
Amesema jitihada hizo zimechangia kuongeza uzalishaji sio tu kwenye korosho bali hata kwa mbaazi na ufuta.
Atakapopewa ridhaa, alisema ataendelea kutafuta masoko ya uhakika sio kwa korosho pekee bali yote, huku akiendelea kuvutia wawekezaji kwa ajili ya kujengwa viwanda vya kuchakata mazao hayo.
“Serikali itaendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi vyama vya ushirika, tutavisimamia kwa ukaribu zaidi, ili kuondoa ubadhilifu wa fedha za wana-ushirika, lakini pia ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima,” amesema.

Amesema dhamira yake ni kuvijenga kuwa taasisi itakayotegemewa katika uendeshaji wa shughuli za kilimo nchini.
Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, amesema Serikali yake itaendelea kupima maeneo ya wafugaji ili kuepusha wasizagae nchi nzima bali wawe katika maeneo maalumu ya kuendelea na shughuli zao.
“Lengo letu ni kwamba tukimaliza miaka mitano ijayo, kila Mtanzania awe karibu na maji safi na salama, hilo ndilo lengo letu kwa hiyo tunakwenda kuifanya hiyo kazi,” amesema.
Kuhusu Mkoa wa Mtwara, amesema ni miongoni mwa mikoa mikongwe ukianzishwa mwaka 1971 na eneo la kimkakati kwa uchumi wa kanda ya kusini.
Kwa sababu hiyo, amesema ndiyo maana Serikali yake imejizatiti kuhakikisha mkoa huo unaunganishwa kwa njia za maji, barabara, reli na anga.
“Ni imani yetu ujenzi wa njia ya reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay, utaturahisishia biashara na wenzetu wa Msumbiji na Malawi,” amesema.
Ameeleza Serikali yake imechochea ukuaji wa Bandari ya Mtwara na tangu uamuzi wa usafirishaji wa korosho ufanyike katika bandari hiyo, makubwa yamefanyika.
“Furaha yangu ni kwamba wenyewe wana-Mtwara wanafurahia hilo, kwamba korosho ya Mtwara isafirishiwe katika Bandari ya Mtwara. Mbali ya korosho, Bandari ya Mtwara ndiyo pekee inayosafirisha Makaa ya Mawe,” amesema



