
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kwa utendaji wake ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ni dhahiri kuwa kazi imefanyika.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo, Alhamisi Septemba 25, 2025 alipozungumza na wananchi wa Lindi Mjini mkoani Lindi katika mkutano wake wa kampeni za urais.
“Hakuna awamu itasema imemaliza kazi yote, lakini kwa kweli katika kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita kazi kubwa imefanyika na kama mtatupa ridhaa ya kuendelea, mengi yaliyoanza hapa tunakwenda kuyamaliza,” amesema.
Mfano wa miradi aliyosema itakwenda kumaliziwa katika kipindi kijacho, amesema ni ufikishaji wa huduma ya umeme katika vitongoji vyote ili kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Huduma ya maji ni changamoto nyingine, aliyoahidi kuimalizia atakapopewa ridhaa ya kuiongoza Tanzania, akisema atahakikisha kila Mtanzania anakuwa karibu na maji, huku vyanzo vikiendelea kutunzwa na kukarabatiwa.
Kwa upande wa sekta ya afya na elimu, amesema Serikali yake itaendelea kujenga vituo vya afya, zahanati na shule kuhakikisha huduma zinasogezwa karibu zaidi na wananchi.
“Ni kweli tunakwenda kuufungua ukanda wote wa Kusini, Lindi, Mtwara mpaka Ruvuma kule,” amesema Dkt Samia na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.







