
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan ameeleza namna pembejeo na mbolea za ruzuku zilivyowezesha kuongeza uzalishaji wa mazao ya ufuta, korosho na karanga wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.
Dkt. Samia ameeleza hayo leo Jumanne Septemba 23,2025 ikiwa ni siku ya kwanza ya kampeni zake mkoani Mtwara akitokea Ruvuma alikohitimisha leo asubuhi eneo la Nakapanya wilayani Tunduru.
Akiwahutubia wananchi wa Mangaka katika mkutano wa hadhara wilayani Nanyumbu, Dkt. Samia ameanza kwa kuwapongeza wananchi wa wilaya hiyo, kwa namna wanavyotumia vizuri mbolea na pembejeo zinazopelekwa.
Mgombea huyo, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema hatua hiyo imewezesha ongezeko la uzalishaji wa zao la korosho kutoka kutoka tani 15,000 za korosho hadi 24,000.
“Hii korosho mara mwisho katika eneo hili, iliingiza Sh. 73 bilioni mikononi mwa wakulima, vilevile katika zao la karanga uzalishaji umepanda kutoka tani 26,000 (Sh. 65 bilioni) hadi tani 33,170 (Sh 82 bilioni) fedha hizi zimeingia kwa wakulima,”
“Katika ufuta uzalishaji umependa kutoka uzalishaji wa tani 1,580 (Sh 3bilioni) na kuvuka malengo ya kuzalisha hadi tani 11,800 (Sh 38.8 bilioni. Hali ndiyo hiyo kwenye mbaazi ambazo zamani ilikuwa mboga, leo ni zao la biashara,” amesema Dkt Samia.
Katika zao la mbaazi, Dkt Samia amesema uzalishaji umepanda kutoka tani 1,130 (Sh 1bilioni) hadi tani 5,950 (10.8 bilioni.)
“Sasa ndugu zangu tukisikia kazi na utu, tunasongea mbele. Kazi hii ya kuleta mbolea na pembejeo kukuza kilimo ili wakulima kupata fedha ziingie mikononi mwao ni kukuza utu wao,”
“Tukijua kuwa fedha hizo zitatumika kujenga nyumba za maana, kusomesha watoto, watatibiwa vizuri, hivyo ndivyo utu wa mtu unavyotunza na kuimarishwa,” ameeleza Dkt Samia na kuongeza kuwa :
“Manufaa yote hayo ni kutokana na ruzuku za mbolea na pembejeo zinazotolewa. Serikali yenu tunaendelea kutatafuta masoko zaidi ili kulinda bei ya mazao haya ambayo kiuhalisia yanategemea soko la kimataifa,” amesema Dkt Samia.





