
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali yake inatarajia kujenga soko la kisasa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumatatu Septemba 22, 2025 alipozungumza na wananchi wa Tunduru wakati wa mkutano wake wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Amesema atajenga soko hilo la kisasa kwa ajili ya wananchi wa Tunduru kufanya biashara zao na hatimaye kukuza uchumi wa eneo husika na watu wake kwa ujumla.
Sambamba na soko, ameahidi pia kujenga maghala matatu ya kuhifadhia mazao na kuongeza skimu mbili za umwagiliaji kwa ajili ya kuwapa nafasi wakulima kufanya shughuli zao bila kutegemea mvua.
“Kuna vitalu 221, vinavyosubiri kutumiwa na wafugaji, tutaleta wawekezaji watumie vitalu hivi, waongeze ajira Tunduru na kukuza uchumi wa wilaya,” amesema.
Kuhusu wanyamapori kuingilia maeneo ya makazi, Dkt Samia amesema ndegenyuki tano zimenunuliwa kwa ajili ya kufukuza wanyama na hilo linafanywa Tanzania kote kwenye changamoto kama hiyo.
