Dkt Samia aahidi kuvalia njuga matibabu ya kibingwa hospitali za Ruvuma

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha huduma za afya Wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa kuongeza vituo vya afya na vifaa tiba.

Dkt Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumatatu Septemba 22,2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake katika Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma.

Amesema akipata ridhaa Oktoba 29,2025 Serikali itajenga tena vituo vingine vya afya viwili vijiji vya Litola na Mchomola na kufikisha idadi ya vitano, sambamba kupeleka magari ya wagonjwa ili kurahisisha kusafirisha wagonjwa.

“Tunapoendelea mbele mkitupa ridhaa tunajipanga kujenga tena vituo vya afya viwili pale Litola na Mchomola, pamoja na vifaa tiba,”

“Tutaleta magari ya wagonjwa ili kusarifisha wagonjwa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali za wilaya au ya rufaa,” amesema Dkt Samia.

Dkt Samia amesema atahakikisha ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma unamalizika ili kurahisisha huduma za matibabu kwa wananchi wa mkoa huo hasa yale ya kibingwa.

“Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma tunakwenda kuimaliza, ili huduma za kibingwa zipatikane ndani ya mkoa, hakuna tena kusafirisha watu kwenda sijui Muhimbili au kwenda wapi…,”

Katika maelezo yake, Dkt Samia amesema mwaka 2024 alifanya ziara ya kikazi wilayani Namtumbo, ambapo alisikiliza kero za wananchi, changamoto na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kujua imefikia wapi,”

“Mara hii tumekuja kuomba kura zenu ili mtupe ridhaa kuendelea kuongoza.Nimekuja kwenu kukiombea CCM kura kwa sababu kinaweza, tumefanya makubwa kwa Tanzania nzima kuanzia sekta za afya, elimu, mbolea na kilimo,” ameeleza.

Dkt Samia amesema kilio kingine alichokumbana nacho kwenye ziara yake mwaka 2024 ni kuhusu shamba la Nafco, kimeshafanyiwa kazi na taasisi hiyo ipo tayari kuachia ekari 3,000 ziende kwa wakulima.

Kuhusu barabara ya kutoka Mtwara Pachani-Nalasi hadi Tunduru yenye urefu wa kilomita 318, Dkt Samia amewaahidi wananchi wa Namtumbo kwamba inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami.

“Sasa ndugu zangu wa Namtumbo, yote yaliyofanyika, yatakayofanyika kuna sababu ya CCM kushindwa hapa? Kuna sababu? Akijibiwa hakuna… na wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *