Dkt Samia kujenga mitambo ya kukoboa kahawa Ruvuma

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo, serikali yake itajenga mitambo ya kukoboa kahawa mkoani Ruvuma ili kuliongezea thamani zao hilo, kabla ya kulipeleka sokoni.

Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo leo, Jumatatu Septemba 22, 2025 alipohutubia katika mkutano wa kampeni za urais, uliofanyika Songea Mjini mkoani Ruvuma.

Amesema katika mkutano wa Januari mwaka huu uliozikutanisha nchi 25 zinazozalisha kahawa, liliwekwa lengo la kufikia mwaka 2035 asilimia 50 ya kahawa bora inayozalishwa Afrika iwe inasindikwa kabla ya kuuzwa.

Ili kutimiza lengo hilo, Dkt Samia amesema mitambo ya kukoboa kahawa kabla ya kuiuza itawekwa mkoani Ruvuma, kuhakikisha zao hilo linaongezwa thamani.

Hatua hiyo, amesema itaambatana na uanzishwaji wa kongani za viwanda zitakazochakata bidhaa na mazao yanayozalishwa katika mkoa husika, yakiwemo madini ya urani, dhahabu na mengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *