Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuipa ndege klabu ya Yanga kwenda kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Lakini pia kila goli litakalofungwa na Yanga katika fainali atatoa milioni 20.
Rais Samia ametangaza uamuzi huo leo Mei 18, 2023 akiwa katika hafla ya uzinduzi wa minara ya kurusha matangazo ya TV ardhini (DTT) ya Azam Media Ltd Jijini Dar es Salaam.
“Serikali itatoa ndege (kwa Yanga) kuwapeleka katika mchezo wa fainali, ndege hiyo itabeba wachezaji, itabeba mashabiki na naomba sana wale viongozi wa TFF muwape moyo kama serikali tunavyofanya. Muwasemee vizuri ili wakapate ushindi”
“Kwa upande wa serikali ni hivyo kuwa tutatoa Tsh. 20 milioni kwa kila goli pamoja na kutoa ndege ya kwenda, itawasubiri pamoja na kuwarudisha” Alisema Rais Samia.
Hii inakuja baada ya Yanga kuweka rekodi kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla kwa timu kutoka Tanzania kufika hatua ya fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.