Samia aahidi uchumi unaokuza ajira na kipato cha mtu mmoja mmoja

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema katika miaka mitano ijayo, Serikali yake itajikita katika kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Amesema atalitekeleza hilo, kwa kuhakikisha anawaandalia wananchi mazingira ya kuwa na shughuli za kufanya ili waingize vipato na kuinua ustawi wa maisha yao.

Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo leo Septemba 18,2025, alipozungumza na wananchi wa Nungwi visiwani Zanzibar, katika mkutano wake wa kampeni za urais.

Amesema serikali yake katika miaka mitano ijayo, inalenga kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja, kwa kuweka mazingira tarakayowawezesha kuwa na shughuli za kufanya.

Mbali na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja, Dkt. Samia amesema CCM katika miaka mitano ijayo, inalenga pia kuinua hali za maisha ya wote, kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu na kujenga taifa linalojitegemea.

“Katika kujenga Taifa linalojitegemea, hatutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania, kila kijana awe na shughuli inayompa kipato, yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja ajitegemee, alafu kwa ujumla wetu tutaweza kujitegemea,” amesema.

Pia, ameahidi kuendelea kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na kuirasimisha sekta isiyo rasmi, ili kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema anapata ujasiri wa kuomba ridhaa ya kuwaongoza tena Watanzania, kwa sababu Serikali yake imefanikiwa kufanya mambo makubwa na inatarajia kuyafanya makubwa zaidi kwa siku zijazo.

Dk. Samia amesema kazi kubwa imefanywa katika sera za kifedha na uchumi na kuleta manufaa kwa pande zote za muungano.

Amesema matumaini yake mwakani ukuaji wa uchumi wa Tanzania utafikia asilimia 7, kama ilivyo upande wa Zanzibar mwaka huu.

Ameahidi kuimarisha uchumi wa buluu na kuhakikisha wananchi wananufaika nao.

Amesema kazi kubwa imefanywa kukuza uhusiano wa kidiplomasia na sasa Tanzania ipo katika nafasi nzuri kimataifa, heshima inayopatikana ulimwenguni ni kwa sababu ya umoja na mshikamano.

Kuhusu ulinzi na usalama, amesema kazi nzuri imefanywa ndiyo maana nchi iko vizuri, huku akisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama viko vizuri kuhakikisha ulinzi wa amani siku ya uchaguzi.

Akizungumzia Muungano, amesema ni lulu ya Afrika kwa kuwa kuna waliojaribu lakini walishindwa.

Amesisitiza Watanzania kuendelea kuuenzi na kuulinda muungano kwa kuwa ni msingi wa amani, umoja na mshikamano.

Amesema CCM inaamini muungano umekuwa na manufaa kwa pande zote mbili, huku akitaka wachache wanaoubeza na kuupotosha umma wapuuzwe.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwa kuwa CCM iliahidi maendeleo na tayari yanashuhudiwa, wananchi wana kila sababu ya kuwachagua wagombea wake.

Amewahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025, kama wanavyojitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *