Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WIMBO wa ‘Oktoba Tunatiki’ ulioimbwa na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’ umemuinua mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, kutoka katika kiti alichokuwa ameketi na kuanza kucheza.
Hii ni mara ya tatu kwa Dkt. Samia kuinuka kutoka katika jukwaa kuu la kampeni na kuanza kuburudika kwa nyimbo za wasanii wanaotumbuiza kwenye majukwaa ya kampeni.
Kwa mara ya kwanza, alicheza wimbo wa ‘Samia Anashindwaje’ ulioimbwa na Harmonize, kisha akacheza tena wimbo ulioimbwa kwa lugha ya kinyakyusa, alipokuwa mkoani Mbeya kwa mkutano wa kampeni.
Leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, Dkt Samia aliinuka tena kutoka katika kiti alichokuwa ameketi na kuwaambia viongozi wengine kuanza kucheza wimbo wa Oktoba Tunatiki, akiwa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar.
Wimbo huo wa Zuchu wenye maudhui ya kuwahamasisha wananchi wamchague Dkt Samia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, ni miongoni mwa burudani pendwa katika majukwaa ya kampeni za CCM zinaendelea.
Pamoja na Dkt Samia, wengine walioinuka na kuanza kucheza wimbo huo ni mwenza wa Rais wa pili wa Tanzania, Mama Siti Mwinyi, mwenza wa Rais wa Zanzibar, Mariam Mwinyi na viongozi wengine.
Viongozi hao pia, waliendelea kuburudika jukwaani hapo hata alipopanda msanii mkongwe wa taarabu, Khadija Kopa aliyeimba wimbo unaoitwa ‘Samia Hajambo.’


