Sababu za nyomi mikutano ya Dkt Samia zatajwa

Na Mwandishi Wetu

NYUMA ya maelfu ya wananchi wanaofurika katika mikutano ya kampeni za Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan kumejificha mengi, wanazuoni wanachambua.

Umati huo mkubwa unaoshuhudiwa, kwa mujibu wa wachambuzi hao, ni ishara ya nguvu ya chama na mgombea husika, mwamko na hamasa ya wananchi, kadhalika mtandao mpana kilionao chama chenyewe.

Mitazamo ya wachambuzi hao, inakuja katikati ya mfululizo wa matukio ya maelfu ya wananchi wanaojitokeza katika mikutano ya kampeni za urais za Dkt Samia, aliyoifanya kwenye mikoa 10 hadi sasa.

Wingi huo wa wananchi wanaohudhuria mikutano hiyo, uliibua minong’ono kutoka kwa baadhi ya watu waliodai, CCM inatumia mbinu ya kuwasafirisha wananchi kwa magari kuwapeleka wakajaze mikutano.

Hata hivyo, Dkt Samia amelifafanua hilo, akisema chama hicho kinasaidia usafiri, lakini wa kuwasafirisha wananchi ndani ya wilaya husika, sio kuwatoa mkoa mmoja kuwapeleka mwingine.

“Lazima tutoe watu, huwezi kutegemea mtu anatoka kilomita nyingi huko 90 au 100 ndani ya Rungwe atembee kwa mguu afike hapa, lazima tuwasaidie usafiri kufika hapa.

“Hilo ni hakika, lakini hatutoi wilaya nyingine kwenda wilaya nyingine tunatoa ndani ya wilaya hiyo hiyo,” alisema Dkt Samia alipokuwa Rungwe mkoani Mbeya katika mkutano wa kampeni ambao pia ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Mwamko kuhusu uchaguzi

Kwa mujibu wa ripoti ya Afrobarometer ya mwaka 2022, asilimia 67 ya Watanzania wanaamini mikutano ya hadhara ya kisiasa ni jukwaa muhimu la kutoa maoni na kusikilizwa.

Hii inaonyesha hatua ya wananchi kuvutiwa na mikutano ya hadhara ni tabia ya Watanzania.

Ripoti ya Afrobarometer, inashabihiana na ile iliyotolewa na Twaweza mwaka 2023, ikionyesha asilimia 74 ya Watanzania hufuatilia kampeni kupitia mikutano ya hadhara.

Ukubwa wa chama, hamasa

CCM, imeasisiwa mwaka 1977, bado kina mtandao mpana zaidi vijijini na mijini kuliko chama chochote nchini, inaelezwa na Profesa Bakari Mohamed wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kinachoelezwa na Profesa Bakari, kinathibitishwa na Ripoti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2020, inayoonyesha mwaka huo, CCM ilikuwa na matawi zaidi ya 16,000 nchi nzima.

“Kwa mtandao huu ndipo tunaona picha za viwanja vilivyofurika watu, mara nyingine wakisafirishwa kwa magari makubwa ya chama au kushawishiwa na hamasa ya kijamii,” anasema.

Uchumi, ahadi na uhalisia

Kwa miaka minne iliyopita, Dkt. Samia amewekeza zaidi kwenye diplomasia ya uchumi na ujenzi wa miundombinu mikubwa.

Benki ya Dunia mwaka 2024, iliripoti ukuaji wa uchumi wa Tanzania ulifikia asilimia 5.1, juu ya wastani wa Afrika Mashariki.

Mradi wa reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Julius Nyerere na Daraja la JP Magugfuli ni mifano ya miradi inayotajwa mara kwa mara kwenye kampeni.

“Ahadi hizi zinapowekwa kwenye jukwaa, wananchi hujitokeza kwa wingi kusikiliza, si kwa sababu wote ni wapiga kura watakaoamua, bali kwa sababu kila mmoja anataka kujua nafasi yake katika mustakabali wa maendeleo,” anaeleza Dk Timoth Lyanga, mwanazuoni wa uchumi.

Uhusiano na ushiriki wa vijana

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) mwaka 2023, vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanaunda takribani asilimia 60 ya wapiga kura nchini.

Dkt. Lyanga anasema hilo ndilo kundi linalojitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni, wakishangilia, kupiga picha na kushiriki kwenye mitandao ya kijamii.

Mvuto wa mgombea

Dkt. Lyanga anasisitiza vvuto wa Dkt Samia unashawishi wananchi kujitokeza kwenye mikutano yake ya kampeni kwa sababu unaunganisha historia yake ya uongozi na umaarufu wa kimataifa.

Anasema nguvu ya mgombea haiishi tu kwenye hotuba za kisiasa, bali pia inatokana na ushuhuda wa utekelezaji wa miradi, uongozi thabiti na sera zinazogusa maisha ya wananchi.

“Ahadi hizi zinapowekwa wazi kwenye jukwaa la kampeni, wananchi hujitokeza kwa wingi, wakitaka kusikiliza moja kwa moja kutoka kwa mgombea husika,” anasema.

Anaeleza wengine huvutiwa na hali ya kumwona mkuu wa nchi mubashara, kwa kuwa si jambo rahisi kumwona kwa karibu tofauti na mikutanoni.

Mikutano ni siasa na tamasha

Huwezi kutenganisha kampeni za uchaguzi na upepo wa burudani unaoambatana nazo. Wanamuziki maarufu, wasanii wa maigizo na vikundi vya sanaa hujipenyeza kwenye majukwaa hayo, kama inavyoelezwa na mchambuzi wa siasa Philemon Mtoi.

“Watanzania wengi hususan vijijini, mikutano ya kampeni ni fursa ya kipekee ya kupata burudani bure na CCM huwa inakuwa na wasanii wengi, ndio maana wananchi wanajitokeza,” anasema Mtoi.

Hii ndiyo sababu katika baadhi ya maeneo, umati unaweza kufika hata maelfu kumi au zaidi, lakini upigaji kura, aghalabu hauendani na idadi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *