Makamu wa Rais na ziara mkoani Arusha, asisitiza ulinzi wa rasilimali za Taifa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha wanatambua na kutumia vema dhamana waliopewa ya ulinzi wa rasimali za taifa zilizopo eneo hilo.

Makamu wa Rais amesema hayo leo Jumanne Mei 16, 2023 wakati wa hafla ya Uwekaji jiwe la Msingi Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zinazojengwa katika eneo la Kaminy Estate – Karatu mkoani Arusha. Amesema ni vema watumishi wa hifadhi zote nchini kutunza rasilimali kwa weledi wa hali ya juu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Aidha amewataka watumishi pamoja na wananchi kuwa macho katika kudhibiti yeyote mwenye lengo la kuhujumu hifadhi pamoja na kuepukana na tabia za kushirikiana na majangili wanaoharibu hifadhi za taifa.

Makamu wa Rais ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuimarisha mahusiano na jamiii hususani jamii ya wafugaji na kutoa wito kwa Mamlaka hiyo kuongeza nguvu katika kuboresha mifugo pamoja na ujenzi wa malambo ya maji kwaajili ya mifugo ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji, kuongeza ubunifu na kujenga misingi mizuri ya kujiendesha kibiashara ili kuweza kupata mapato Zaidi na kufikia malengo yaliowekwa.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi wa Ofisi hizo nje ya eneo la hifadhi una lengo la kuondoa shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikiendelea katika eneo la hifadhi. Aidha ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria kanuni na taratibu ili kuepusha migogoro inayotokana na uvamizi katika maeneo ya hifadhi na ujenzi katika mapitio ya wanyama. Ameongeza kwamba Wizara inaandaa programu kupitia vyuo vya wanyamapori itakayosaidia kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza changamoto za migogoro baina ya wananchi na wahifadhi katika maeneo yote nchini.

Waziri Mchengerwa ameongeza kwamba zoezi la kuhamisha wananchi katika eneo la hifadhi la Ngorongoro linaendelea kuratibiwa vema na Wizara na linatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Awali akitoa taarifa za Ujenzi wa Ofisi hizo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro Elibariki Bajuta amesema chimbuko la mradi wa Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kutokana na tishio la kutoweka kwa bionuai,urithi wa utamaduni na rasilimali za miamba kunakochangiwa na ongezeko la watu na mifugo ndani ya hifadhi pamoja na shughuli za kibinadam. Amesema mpango wa ujenzi huo unalenga kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi, kuongeza ufanisi katika kuhudumia wateja pamoja na kuwa mfano katika kuzuia shughuli zote za kibinadamu ndani ya hifadhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *