
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema atahakikisha amani na utulivu vinatawala katika msimu wote wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika kauli yake hiyo, amewasihi wananchi kufuata utaratibu uliowekwa wa kupiga kura na kurudi nyumbani, kwa kuwa uchaguzi ni tendo la kidemokrasia na sio vita.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo jana, Jumatano Septemba 17, 2025 alipozungumza na wananchi wa Makunduchi visiwani Zanzibar, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais, alioufanyia katika Uwanja wa Kajengwa.
“Uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, ni watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa, kuweka kura zetu rudi nyumbani katulie ili nchi ibaki salama,” amesema.
Amewataka wananchi visiwani humo, kuhakikisha katika uchaguzi wanadumisha amani na utulivu, kwani tukio hilo sio tendo la vita.
Dkt Samia amesema baada ya kuapishwa kuwa Rais, alikutana na wazee wa Pemba, pamoja na mambo mengine walimwelekeza kuhakikisha anadumisha amani na utulivu, jambo ambalo ameapa kuhakikisha linatimia.
“Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho, muda wote kushika silaha yoyote, iwe ya moto au ya kimila hakuleti suluhisho la maana. Niwaombe sana wote wanaotusikiliza, amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine yote hasa wakati huu wa uchaguzi,” amesema.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, vimejipanga vema kulinda nchi.
“Sasa hutaki kishindo kapige kura rudi nyumbani tulia, tumejipanga vema. Kwa hiyo nisisitize suala la amani na utulivu,” amesema Dkt Samia.
Sambamba na hayo, Dkt Samia amesema maendeleo ni hatua hivyo kila Serikali inafanya panapostahili, nyingine inaendelea palipoishia.
Amesema kwa kuwa mazingira na watu hubadilika, kila wakati mahitaji huongezeka, hivyo si rahisi kumaliza matatizo yote kwa wakati mmoja.
Kuhusu muungano
Amesema Serikali yake imefanikiwa kuuenzi muungano ulioasisiwa na wakongwe Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Ameeleza muungano umekuzwa katika nyanja za kiuchumi na kisiasa na sasa umekuwa wa kindugu kuliko vigezo vingine vyote.
“Hizi ndizo tunu kuu na msingi kwa maendeleo ya Taifa letu na hizi tutazilinda kwa bidi kubwa. Tunakwenda kulinda tunu ya muungano, amani na utulivu,” amesema.
Amesema atakapopewa ridhaa, anatarajia kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili wageni kutoka nje waende kusoma.
Katika mkutano huo, amesema ni jukumu la wagombea wa nafasi zote kupita na kuwaeleza watu yaliyofanyika ili wananchi wajue na waamue kuichagua CCM kwa kuwa ndio inayoleta maendeleo.
Ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ndiyo yaliyompa nguvu ya kujiamini na kuomba ridhaa kwa wananchi ili aiongoze tena Tanzania.








