Benki ya TCB yazindua hatifungani mpya ‘Stawi Bond’

-Thamani yake ni Sh. bilioni 50

-Yalenga kuwakomboa wajasiriamali wadogo na kati

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua hatifungani mpya ya miaka mitano ijulikanayo kama Stawi Bond, yenye thamani ya Sh. bilioni 50.

Hatifungani hii inalenga kukusanya fedha zitakazotumika kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa riba nafuu.

Stawi Bond inatoa riba ya kuvutia ya asilimia 13.5 kwa mwaka, ambayo itakuwa inalipwa kila baada ya robo ya mwaka. Hii ni fursa ya pekee kwa Watanzania kuwekeza huku wakipata faida ya uhakika. Kiwango cha chini cha kuwekeza ni shilingi laki tano, hatua inayowezesha idadi kubwa ya wananchi kushiriki kwenye soko la mitaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amesema kuwa Stawi Bond ni zaidi ya chombo cha kifedha.

Ameeleza kuwa hatifungani hiyo inafungua njia mpya ya wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye uwekezaji wa taifa na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa pamoja.

Mwandumbya amebainisha kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kisera ili taasisi za kifedha ziweze kuja na ubunifu unaowawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mikopo kwa gharama nafuu.

Ameongeza kuwa hatua hii inakwenda sambamba na jitihada za serikali za kuimarisha uchumi na kupunguza utegemezi wa mikopo ya kigeni.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo, amesema fedha zitakazopatikana kupitia Stawi Bond zitaelekezwa moja kwa moja katika kusaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Ameeleza kuwa lengo ni kupanua mtaji, kupunguza gharama za mikopo na kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma za kifedha.

Amesisitiza kuwa, Stawi Bond inaleta suluhisho la kweli kwa wafanyabiashara wadogo, kwasababu itawawezesha kupata mikopo nafuu na hivyo kukuza shughuli zao.

“Hii pia ni sehemu ya mkakati wetu wa kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wengi zaidi,” amesema Mihayo.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, amesema Stawi Bond ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza benki ya serikali kutoa hatifungani ya aina hiyo.

Ameeleza kuwa hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Ufadhili Mbadala wa Miradi, unaolenga kuzisaidia taasisi za umma kutumia masoko ya mitaji badala ya kutegemea bajeti pekee.

Mkama pia alifafanua kuwa thamani ya masoko ya mitaji nchini imeendelea kukua kwa kasi.

“Katika kipindi cha miaka minne, thamani hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 75 kutoka Sh. trilioni 31.64 mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 55.45 mwezi uliopita,” amesisitiza.

Amesema ongezeko hilo linaonyesha ubunifu, uthabiti na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela, amesema Stawi Bond imezinduliwa kwa wakati muafaka kwasababu sasa wananchi wanaweza kuwekeza kwa urahisi kupitia mifumo ya kidigitali.

Amebainisha kuwa uwekezaji unaweza kufanyika kupitia app za TCB na DSE, hatua inayorahisisha ushiriki kutoka popote nchini.

Nalitolela amesisitiza kuwa hatifungani hii ni fursa muhimu kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Ameeleza kuwa kuwekeza katika Stawi Bond ni njia ya kuunga mkono maendeleo ya taifa kupitia masoko ya mitaji, huku pia ikiwapa wawekezaji kipato cha uhakika.

Uzinduzi wa Stawi Bond unaashiria mwelekeo mpya wa kifedha nchini Tanzania.

Ni hatua inayolenga siyo tu kuimarisha upatikanaji wa mitaji nafuu kwa wajasiriamali, bali pia kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji, kuimarisha mapato ya serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *