Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Godfrey Chongolo Jana tarehe 15 Mei, 2023 alifanya ziara ya siku moja wilayani Bukombe mkoa wa Geita.
Katika ziara hiyo, Ndugu Chongolo alizindua majengo mbalimbali ya Chama Cha Mapinduzi wilayani Bukombe ikiwemo ukumbi wa mikutano, nyumba ya kupumzika wageni (Rest House) na mgahawa (Restaurant).
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayesimamia Oganaizesheni Ndugu Issa Ussi Gavu.
Katika taarifa iliyotolewa na Afisa Habari kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu Ndugu Said Nguya imeeleza ziara hiyo ni mwendelezo wa CCM kujiimarisha kiuchumi kwa kuendelea kujijenga na kuzindua vitega uchumi vyake ambavyo vitakifanya Chama kuwa imara kiuchumi na kukwepa kutegemea wahusani kujiendesha pamoja na kutumia ziara hizo kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Akizindua ukumbi wa mikutano na kuweka jiwe la msingi nyumba ya kupumzikia wageni Bukombe amewatadharisha wale wote wanaohangaika na kujipitisha kwa wananchi kutaka uongozi hasa ubunge na udiwani kuacha mara moja kwani wanakiuka Katiba na miongozo ya Chama.
“Niwaambie tu wale wote wanaohangaika kwenye majimbo na kata kutafuta Ubunge na udiwani waache. Tunawaona na tutawachukulia hatua za kinidhamu. Chama hiki kina taratibu zake na muda wa siasa bado kwasasa tuwaache wale waliochaguliwa wafanye kazi yao mpaka hapo muda utakapofika ndipo kila mwanachama ataruhusiwa.” Alisema Chongolo.