
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIKA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025, Kampuni ya Media Brains kwa udhamini wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kutoka Ujerumani, wamewakutanisha pamoja waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam kuwapa mbinu za kuripoti kwa kuzingatia haki na usawa.
Aidha, wamewapitisha waandishi wa habari katika Sheria Mpya ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Sheria Mpya ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili kuwajengea uwelewa wa pamoja namna wanavyoweza kuripoti habari kwa weledi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Media Brains, Jesse Kwayu, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja, amesema tafiti zinaonyesha kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, wagombea wanawake walipata nafasi ndogo kwenye vyombo vya habari ikilinganishwa na wanaume, hivyo kunahitajika usawa katika uchaguzi wa mwaka huu.
Aliwaasa waandishi wa habari kuzingatia misingi na weledi ya waandishi wa habari katika uchaguzi mkuu kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi na kulinda amani.
Naye Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains Absalom Kibanda, amesisitiza umuhimu wa wanahabari kusoma kwa makini sheria hizo ili kuwapa uelewa mpana na kuwaelimisha wananchi.
“Sheria hizi zimeanza kutumika kwenye mchakato wa awali wa uchaguzi. Ni muhimu wanahabari wakazifahamu ili kujilinda kisheria na kutekeleza majukumu yao kwa weledi,” amesisitiza Kibanda.
Naye Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, Neville Meena, amedokeza kuwa, uelewa wa sheria utasaidia wanahabari kuepuka makosa, hasa wanapowahoji wagombea na wadau wa uchaguzi.
Mafunzo hayo pia yamehimiza uhakiki wa habari kabla ya kuchapishwa ili kuepuka taharuki na kuchochea migogoro na machafuko.
“Waandishi wa habari tunapaswa kufanyakazi zetu kwa mujibu wa sheria, zipo sheria zinazohusu uchaguzi na zingine zinatugusa sisi waandishi moja kwa moja yaani maadili na miiko yetu hivyo tumekutana ili kukumbusha sheria hizi ili tufanyekazi zetu kwa weledi,” amesema Meena
Aidha, amesema Kampuni ya Media Brains tayari imeshatoa mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari katika mikoa ya Mbeya, Kigoma, Mwanza, Kilimanjaro, Pwani na Morogoro na kwamba wanadhani ule ujumbe walioufikisha watauzingatia wakati wa kuripoti habari hizo za uchaguzi.


