Mhandisi Manyanga: Mradi wa TACTIC utabadilisha Mji wa Musoma

Na Mwandishi Wetu, Musoma

SERIKALI kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeingia makubaliano ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi katika Manispaa ya Musoma chini ya Mradi wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC), unaofadhiliwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 410.

Mikataba ya ujenzi imesainiwa leo katika hafla iliyofanyika mjini Musoma, ikihusisha ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Kisasa ya Bweri, Soko la Kisasa la Nyasho, na barabara kadhaa za mjini zenye urefu wa zaidi ya kilomita 3, ikiwemo Mukendo, Shabani na Musoma Bus–Saanane.

Mkandarasi anayetekeleza kazi ni kampuni ya Henan Highway Engineering Group Company Limited, kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 19.9 bila VAT na utekelezaji unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 kuanzia Agosti 15, 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Emmanuel Manyanga, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TARURA, amesema miradi inalenga kuboresha huduma za usafiri na biashara, kupunguza changamoto za mafuriko, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Musoma.

Baada ya kukamilika, Stendi ya Bweri itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 42, daladala 50, bajaji 50 na pikipiki 20, sambamba na uwapo wa kituo cha polisi, maeneo ya mapumziko na mifumo ya kisasa ya maji na nishati.

Soko la Nyasho litakuwa na maduka 260, vizimba 432 na eneo la migahawa kwa mama lishe hadi 100, kituo cha polisi na miundombinu bora ya kuhifadhi mazingira, huku mapato ya manispaa yakitarajiwa kuongezeka kutoka Sh. milioni 57 kwa mwaka hadi kufikia Sh. milioni 250.

Mradi wa TACTIC unatekelezwa katika miji 45 nchini, ukiwa na malengo ya kuboresha miundombinu, kuimarisha mipango miji na kuongeza ushindani wa kiuchumi wa Halmashauri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *