
MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, ameongoza hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya uboreshaji miundombinu katika Manispaa ya Musoma chini ya Mradi wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness Project (TACTIC), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kanali Mtambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia Musoma miradi hiyo muhimu itakayogharimu Sh. bilioni 19.975 (bila VAT) na ambayo inalenga kuboresha miundombinu ya barabara, masoko na vituo vya mabasi.
Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mkendo, Shaabani na Musoma–Saanane, pamoja na ujenzi wa Soko Kuu la Nyasho na Kituo cha Mabasi cha Bweri.
Mhe. Kanali Mtambi alisema miradi hiyo ikikamilika itabadilisha mandhari ya mji wa Musoma, kuwa kivutio kipya na kuchochea uchumi wa eneo hilo, sambamba na kutoa ajira kwa wananchi hususan vijana na wanawake.
Aidha, ametaja miradi mingine mikubwa inayoendelea Musoma ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma na miradi ya maji safi na salama ambayo kwa sasa imefikia asilimia 98 ya upatikanaji.
Ametoa wito kwa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuhakikisha miundombinu inayojengwa inatunzwa na kuwataka wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati na kwa viwango bora, akisisitiza kuwa serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wake.
Pia aliwataka wananchi kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na miradi hiyo, ikiwamo huduma kwa watalii na Wafanyabiashara watakaotumia Musoma mara baada ya uboreshaji kukamilika.



