Na Sarah Moses, Dodoma.
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) yametakiwa kuwa na rasilimali fedha ili kuepukana na kuwa tegemezi kutoka kwa wadau wa maendeleo na kuendeleza jitahada zake kwa kujitegemea.
Hayo ameyasema leo Agosti 12,2025 Jijini hapa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati alipokuwa akifungua majadiliano mbalimbali kwenye warsha ya kongamano la mashirika yasiyo ya kiserikali .
Amesema kuwa sheria zinaruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kujihusisha na shughuli za kiuchumi kujitafutia fedha kwaajili ya kujiendeleza na sio kugawana fedha hizo.
“Mnapaswa kutekeleza miradi ya uzalishaji ambayo ni endelevu na kuondoa utegemezi kutoka kwa wafadhili, kwa sababu kwa sasa Sera za nchi za Ulaya na Marekani zimebadilika” amesema.
Katika hatua nyingine Dkt. Jingu amesema Mashirika hayo yanawajibu wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kifikra na maendeleo katika jamii kupita utekelezaji wa miradi yao mbalimbali.
“Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali, yamesajiliwa kisheria kwa lengo la kutoa huduma na elimu katika nyanja tofauti kwa jamii hivyo mtambue kwamba ajenda ya maendeleo endelevu katika Taifa ni pamoja na kuwa mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii”amesema.
Kwaupande wake Mkurugenzi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Esta Msambazi ambaye ni Msajili Mashirika ya Msaada wa Kisheria Tanzania akizungumzia mada mbalimbali zilizojadiliwa katika kongamano hilo amesema mashirika takribani 300 yamesajiliwa kutoa msaada ya kisheria.
“Kuanzishwa kwa msaada wa kisheria Mama Samia legal Eid Campaign wananchi zaidi ya millioni 34 wamefikiwa na migogoro 26,000 imeripotiwa huku migogoro zaidi ya 6,000 ikitatuliwa” amesema.
Mwisho.