Sarah Moses, Dodoma.
TANZANIA inaweza kuwa mzalishaji wa chakula siyo Afrika tu lakini inaweza pia kuchangia kwa kiwango kikubwa sana duniani.
Hayo ameyasema leo Agosti 6, 2025 Jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara Dkt Suleiman Serera wakati alipotembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonesho ya viwanja vya nane nane ambapo alisema kwa sasa uongezaji wa thamani kwenye bidhaa mbalimbali umeongezeka sana.
Amesema kuwa wameona bidhaa mbalimbali za Tanzania zinazotokana na kilimo jinsi zilivyoongezwa thamani na ubora ambao upo ni ule ambao wameuona kwenye nchi mbalimbali lakini kwa sasa ubora huo unapatikana nchini Tanzania.
“Na hii inatuonyesha kwamba hata dira iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo itaanza kutumika baada ya mwakani tunaona kwamba tunaelekea sasa katika njia ambayo ni sahihi kwenda kwenye kipato cha nchi yetu cha dola tril 1 nahiyo isingewezekana kama hatujaanza na msingi fulani” amesema.
Pia amesema kuwa kila mmoja anachokifanya ni kuhakikisha anaboresha kwenye ule mnyororo wa thamani na kuhakikisha kwamba kilimo na maonesho yenyewe yanakuwa mazuri.
“Wakulima niliowatembelea wengi wamekuwa wakizungumza kwanzia mbegu za asili hawazungumzii changamoto bali wanazungumzia hatua waliyotoka na namna ya nini kifanyike ili waweze kwenda mbele zaidi” amesema.
“Mfano wadau wa mbegu tumeona wanakiri kwamba Serikali imeweza kuwasaidia kusajili mbegu zao nyingi za asili na wanajua kwamba serikali kupitia TOSCI inakwenda kusajili mbegu zingine” amesema.
Amesema wadau hao nao wanaeleza zile jitihada kubwa zilizofanywa na serikali na hivo inaonyesha ushirikiano ni mkubwa kwani siku za nyuma ilikuwa ukienda kwa wale wenzetu ambao hawatokani na serikali hawajui hata ile mipango ya nini kinachoendelea.
Kwahiyo inaonyesha kwamba wanayokazi serikali yakuendelea kushirikisha kama ambavyo wamekuwa wakishirikisha na wameona kwamba katika kushirikisha huko kumeweza kusaidia zaidi.
Hata hivyo amesema hata kwenye vyombo vya habari mbalimbali wamekuwa wakitaka kuonyesha jinsi mambo yanavyoendelea katika maonesho hayo tofauti na wakati ule ambapo vyombo vya habari vilikuwa vikichagua mahali pa kwenda.
Mwisho.