Bei ya njiwa wa mapambo sawa na kilo 100 za mchele

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

KWA wengi njiwa ni kitoweo na hufugwa kwa mapenzi si biashara. Lakini Deogratius Temba, kijana kutoka Dodoma, Tanzania amebadilisha dhana hiyo. Anafuga njiwa wa kipee.

Hawa ni njiwa wanaojulikana kama njiwa wa mapambo ambao hutumika kupendezesha makazi, maofisi ama sehemu zingine kama mahoteli na za kupumzikia.

Kati zaidi ya aina 10 ya njiwa wa mapambo alionao Deogratius, mmoja anauzwa kati ya Dola za Kimarekani 85 mpaka $180 au shilingi laki 4 za Tanzania.

Unaweza kujiuliza wanafananaje njiwa hawa, na kwanini kijana huyu maarufu kama Deo Manjiwa ameamua kuwafuga njiwa hawa wa mapambo? Mwandishi wetu Yusuph Mazimu alimtembelea huko Dodoma kujua mengi.

Historia ya Njiwa hawa

Ufugaji wa njia ulianza miaka zaidi ya 5,000 iliyopita. Njiwa walifugwa kienyeji na kawaida. Wafugaji waliwafuga kwa madhumuni tofauti ikiwemo kutumika kama kitoweo, baadhi kuwatumia kupeleka ujumbe (vikaratasi ama kufika kwao), wakifundishwa kwa namna mbali mbali.

Lakini katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ufugaji wa njiwa kama ‘hobby’ au kwa kujifurahisha ama kwa kupenda kulianza kushika kasi na sasa karibu kila mahali ufugaji huu na ule wa kibiashara umeanza kushika kasi.

“Wakati nataka kuanza kuwafuga hawa njiwa majirani hawakuwa na shida ila mke. Shida ilikuwa kwa mke wangu, Kwa sababu wakati nataka niwanunue mke wangu aligoma kabisa,” anasema Deo Manjiwa na kuongeza: “Alisema unanunua njiwa milioni 1,200,000 ni njiwa gani, nikamwambia wewe tulia utawaona.”

‘Wanakula kama mchwa’

Tofauti kubwa ya njia hawa wa mapambo iko kwenye maeneo manne. Ulaji wao, maisha yao, muonekano wao na kustahili kwao ugumu wa mazingira.

Wana muonekano mzuri wa kupendeza. Muonekano unaobebwa na rangi zao, muundo wa maumbo yao, manyoya yao yaliyokaa na namna wanavyotembea. Na hiki kinawatofautisha na njiwa wengine wa kawaida. Njiwa wa asili.

Hawa hawaweza kuvumilia mazingira magumu. Lakini ukiwaweka kwenye mazingira ya ‘kizungu’, wanaweza kuzaliana sana na kuishi kwa wiki. Ndani ya mwaka mmoja Deo Manjiwa amefanikiwa kuzalisha mamia ya njiwa kutoka njiwa 6 tu alioanza nao.

Ukiacha magonjwa ya mafua kama wanavyoumwa njia wengine, Deo analalamika tu ulaji mkubwa wa njiwa hawa.

“Na hawa kwa siku wanaweza kula kilo tano au nne,” anasema.

Ulaji huu unamtisha mmoja wa watu waliokuja kushangaa njiwa hawa nyumbani kwa Deo Manjiwa, eneo la Makole, Dodoma.

“Wanakula kama mchwa, kilo tano si mmekula famila wiki nzima,” anasema Mariam huku akicheka.

‘Njiwa ni Biashara kubwa’

Deo Manjiwa anathibitisha njiwa ni biashara kubwa. Alianza na mtaji wa njiwa sita tu kutoka Zanzibar. Sasa ana mamia ya njiwa wenye thamani ya zaidi ya milioni 25 za kitanzania sawa na dola karibu 10,000 za Marekani.

“Njiwa wote hapa tukiwauza kwa shilingi za Kitanzania 200,000 labda tuseme wako njiwa 100. Laki mbili mara mia inakuja milioni 20. Lakini kila 200,000 ukiziweka kwa gharama za mchele wa sasa hivi unapata kilo 66. Na kilo 66 kwa familia ya watu wanne au watano wanaweza wakala kilo 1. Kwa hivyo thamani ya njiwa mmoja ya 200,000 inaweza kulisha familia kwa miezi miwili. Kwa hiyo njiwa sio mapambo tu njiwa pia ni kipato,” anasema.

Lakini kwa bei ya mchele kijijini isiyozidi 2,500 kwa kilo, njiwa anayeuzwa shilingi laki 4 za kitanzania anaweza kukupa zaidi ya kilo 100 za mchele.

Wanaliwa?

Kwa mujibu wa Deo Manjiwa, ni njiwa wanaoliwa kama njiwa wengine. Tena kwa sababu ni wakubwa kwa maumbo, wapo wanaofikia maumbo kama kuku wa kawaida, ni wazuri kwa familia.

“Huwa nawachinja sana, hasa wale wenye rangi ambazo naona sokoni hazitavutia au wanaoumwa,” anasema

Ila hapendi kufanya hivyo kwa sababu ya thamani yao “Yaani njiwa wa Shilingi 400,000 umchinje tu?” anahoji Deo huku akiendelea kuwahudumia njiwa wake kwenye mabanda yake mawili makubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *