
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selamani Jafo, amesema kuwa ndani ya muda mfupi Tanzania haitahitaji tena kuagiza bidhaa muhimu kama mabati, vioo, nondo na saruji kutoka nje ya nchi, kutokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Jafo Julai 31, 2025 wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan katika mkoa wa Pwani, ambapo alizindua rasmi Kongani ya Viwanda ya Kwala pamoja na Bandari Kavu ya Kwala.
“Kwa mfano, mahitaji ya mabati kwa mwaka ni tani 130,000. Leo hii, kampuni zote zinazozalisha mabati nchini, ikiwamo Lodhia, King Lion, Alaf na mengineyo, yamefikia uzalishaji wa tani 260,000 kwa mwaka. Hii ina maana tunakuwa na ziada ya tani 130,000,” amesema Jafo.
Ameongeza kuwa, hatua hii ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, kuhakikisha kuwa Tanzania inajenga uchumi wa viwanda unaojitosheleza kwa bidhaa za msingi, huku pia ikiongeza uwezo wa kusafirisha bidhaa nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, eneo la Kwala lina zaidi ya hekta 1,000, ambapo zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa kwa uwekezaji unaozidi Dola za Marekani bilioni 3.
Inakadiriwa kuwa bidhaa zitakazozalishwa kwenye kongani hiyo zitaweza kuingiza jumla ya Dola bilioni 6 kwa mwaka, ambapo Dola bilioni 4 zitabaki kwa matumizi ya ndani, na dola bilioni 2 zitatokana na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Waziri Jafo anasisitiza kuwa Wizara itaendelea kusimamia maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa bidhaa Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani.
