Wapigakura milioni 37 wamejiandikisha kupiga kura

Na Sarah Moses, Dodoma.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema jumla ya Wapiga Kura 37,655,559 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Hayo ameyasema leo Julai 26,2025 jijini Dodoma Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati alipokuwa akitangaza ratiba ya Uchaguzi wa Rais ,Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Amesema kuwa idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwa kwenye Daftari, mwaka 2020.

Akizungumzia upande wa Zanzibar, alisema Wapiga Kura 725,876 wapo katika Daftari la Wapiga Kura la ZEC na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.

Katika idadi ya wapiga kura 37,655,559 waliopo katika Daftari, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na Wapiga Kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar.

“Kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69, na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu”amesema.

Wakati huo huo  Mwenyekiti Mwambegele ametaja idadi ya vituo vya kupigia kura kwa Uchaguzi Mkuu wa  2025   kuwa jumla ya vituo 99,911 vitatumika kupigia kura kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Amesema Vituo 97,349 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Bara, na Vituo 2,562 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar.

“Idadi hii ya vituo 99,911 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020”amesema.

Hata hivyo amebainisha kuwa idadi ya vituo 1,766 vilivyopo sasa kwa mujibu wa Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ni sehemu ya vituo vitakavyotumiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge kutoka Zanzibar.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *