Magnet Youth Academy yang’ara kimataifa nchini Ureno, Uswisi

Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Kukuza Vipaji vya Soka cha Magnet Youth Sports Academy, kimepeperusha vyema Bendera ya Tanzania baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano mawili ya kimataifa ya soka kwa vijana ya Iber Cup nchini Ureno na Gothia Cup nchini Uswis, yaliyofanyika mwezi huu.

Kituo hicho kiliwakilishwa na jumla ya watu 80 wakiwemo wachezaji, makocha, na wasaidizi.

Safari hiyo ya kimataifa haikuishia tu kwa ushindi bali pia ilivutia makocha, mawakala wa kutafuta vipaji (scouts) na mashabiki barani Ulaya.

Magnet ilianzia jijini Lisbon katika mashindano ya Iber Cup yaliyofanyika kuanzia Julai Mosi hadi 6, Estoril.

Timu hiyo iliwakilishwa na timu nne za vijana katika makundi ya umri wa miaka U-10, U-11, U-13, na U-17.

Timu hizo zilicheza soka ya kuvutia, zikishinda na kutoka sare dhidi ya wapinzani wao.

Timu ya U-11 iliweka rekodi ya kipekee kwa kufika hatua ya robo fainali, ikionesha dhamira ya academy hiyo katika kukuza vipaji kuanzia ngazi ya chini.

Timu ya U-17 nayo ilipambana vikali kabla ya kutolewa kwa mabao 3-2 katika mechi ya mchujo dhidi ya Barcelona Academy (Dubai).

Wachezaji wa Kituo cha Kukuza Vipaji vya Soka cha Magnet Youth Sports Academy, wakiwa katika picha ya pamoja na Kocha wao, Bizoo Matuka (kushoto)

Ingawa walipoteza, wachezaji walionesha ustadi mkubwa, nidhamu na mshikamano uliowavutia mashabiki na maofisa wa mashindano.

Baada ya mashindano ya Ureno, Magnet waliendelea na safari yao hadi Uswis, ambako timu ya wavulana ya U-17 ilishiriki mashindano maarufu ya Gothia Cup yanayojulikana kama “Kombe la Dunia la Vijana” yaliyofanyika Gothenburg kuanzia Julai 13 hadi 19.

Timu ilifika Julai 7 kwa ndege hali iliyowapa muda wa kuzoea mazingira na hali ya hewa, kwa msaada mkubwa wa Watanzania wanaoishi Gothenburg waliowakaribisha na kuwahamasisha vijana hao.

Maandalizi hayo ya mapema yalizaa matunda. Timu ya Magnet U-17 ilicheza kwa kasi ya kuvutia na kufika nusu fainali.

Waliibuka na ushindi mnono kwenye mechi za mchujo zikiwemo ushindi wa 4-0 dhidi ya timu kutoka Ujerumani, 4-0 dhidi ya Venezuela na 3-0 dhidi ya klabu ya Uswis.

Mchezo wao wa kushambulia kwa kasi uliwafurahisha mashabiki na kuvutia makocha na scouts kutoka kote duniani, jambo lililoongeza heshima ya kimataifa ya academy hiyo.

Siri ya mafanikio yao ilikuwa ni mchanganyiko wa ulinzi imara na mashambulizi ya kasi. Kipa Nibras Ally aling’ara kwa utulivu wake na uwezo wa kuzuia mashuti, huku akimaliza kila mechi ya mchujo bila kuruhusu bao.

Nahodha Junior Jr Michael aliyepewa jina la utani ‘Ukuta wa Berlin’ aliongoza safu ya ulinzi kwa uimara na uongozi wa mfano.

Mshambuliaji Shafii Mbogo alivutia kwa umaliziaji wake na mbinu uwanjani. Kiungo Paul Mhoro alitawala mchezo kwa akili na maono, huku Thierry Murunga akihangaisha mabeki wa upande wa kushoto kwa kasi yake, chenga na krosi sahihi.

Pamoja na mafanikio hayo, Magnet walitolewa hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa 2-1 na timu kali ya Prep School kutoka England.

Mechi hiyo, ambayo ilikuwa ya tatu kwa siku hiyo, iliwachosha vijana kimwili lakini waliendelea kuwa na fahari kubwa. Kocha mkuu aliielezea mechi hiyo kuwa “jioni ya damu na jasho,” ikionyesha changamoto za kimwili na kihisia za soka la vijana la kiwango cha juu.

Timu hiyo ilitoa shukrani zake kwa wote waliowezesha safari hiyo kufanikiwa.

Akizungumza baada ya mashindano, Kocha Mkuu, Bizoo Matuka aliwapongeza wachezaji wake kwa ukuaji na mafanikio.

“Mwaka jana tulifika robo fainali, mwaka huu tumeingia nusu fainali. Ni hatua kubwa mbele. Tumejifunza mengi na tutarudi tukiwa imara zaidi. Malengo yetu ni ubingwa mwakani,” alisema.

Ushiriki na mafanikio ya Magnet Youth Sports Academy katika mashindano hayo mawili makubwa umeonyesha kuwa vijana wa Kitanzania wana vipaji na uwezo wa kushindana na kushinda kwenye jukwaa la dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *