Na Sarah Moses, Dodoma.
MKOA wa Mara umezalisha dhahabu yenye uzito wa tani 58.90 ikiwa na thamani ya shilingi trilioni 6.90 kutoka kwa wachimbaji wakubwa, wakati na wadogo.
Hayo yamebainishwa Julai 18 Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita .
Amesema katika kipindi hicho Serikali imekusanya maduhuli ya shilingi bilioni 568 kutokana na malipo ya mrahaba, ada ya ukaguzi kwenye mauzo ya madini, ada za leseni na tozo mbalimbali za vibali, ushuru wa huduma katika Halmashauri na kodi ya zuio inayokatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Aidha katika Sekta ya Madini kuna urudishwaji wa faida kwa jamii kutoka kwa wamiliki wa leseni na kampuni za uchimbaji madini (CSR). Kwa miaka hii minne kumekuwa na utekelezaji wa miradi 398 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 33.81 zitokanazo na CSR ya sekta ya madini.
“Katika kipindi hiki Serikali imeboresha majengo ya utawala kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi”
Katika hatua nyingine amesema kuwa Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini ikiwemo dhahabu, fedha, shaba, chuma, madini ya ujenzi, madini ya viwandani na madini ya vito. Madini ya dhahabu ndio yanayochimbwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na madini mengine.
Hadi kufikia Juni, 2025 Mkoa ulikuwa na lesseni 2,288 ambazo zinahusisha uchimbaji wa madini, utafiti, uchenjuaji na biashara ya madini.
Aidha, Mkoa kwa kushirikiana na Tume ya Madini na Mgodi wa Barrick North Mara umewawezesha upatikanaji wa lesseni 104 kwa vikundi 48 vyenye jumla ya Vijana 1,836 kutoka vijiji 13 katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
“Uwezeshaji wa makundi hayo ni semehu ya utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) na una lengo la kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini”
“Vijana hao wanapatiwa elimu kuhusu uchimbaji wa madini chini ya uangalizi wa Mgodi wa Barrick North Mara, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Ofisi ya Madini Mkoa”
Serikali imetoa miongozo ya kuyawezesha makundi mbalimbali katika jamii kuweza kuimarisha uwezo wao wa kushiriki shughuli za maendeleo na kuleta usawa wa kiuchumi katika jamii.
“Katika kipindi hiki, kuna ongezeko la vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri za Mkoa wa Mara kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka vikundi 187 mwezi Novemba, 2020 hadi vikundi 324 Aprili, 2025”
Aidha, fedha zinazotolewa kama mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.63 Novemba 2020 hadi shilingi bilioni 5.88 mwaka 2025.
Mwisho.