Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKA la Posta Tanzania, limeingia makubaliano na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuwa wasafirishaji wakuu wa bidhaa na wafanyabiashara mbalimbali katika wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyopangwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yamefanyika leo wakati wa usainishaji wa makubaliano hayo baina ya Postamasta Mkuu, Macrice Mbodo na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis.
Mbodo amesema ushirikiano huo kati ya Posta na TanTrade unafaida kubwa kwa waoneshaji, wananchi na sekta ya biashara kwa ujumla.
Amezitaja faida hizo kuwa ni kuipatia jamii fursa mpya za uchumi ambapo wafanyabiashara wadogo na wa kati watafaidika kwa kupunguza gharama na muda wa kusafirisha bidhaa zao kwenye eneo la maonyesho.
Amesema kupitia huduma hiyo, wafanyabiashara hao wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao kwa wateja wengi, ikiwa ni pamoja na wageni wa kimataifa.
Pia amesema faida nyingine ni kurahisisha usafiri kwa wateja kupitua huduma za Swift Pack na Baggie na kurahisisha huduma za maonesho.
“Pia tutafanya kazi za ‘clearing and forwarding kwa washiriki wa kimataifa. Huduma hii ya Cargo ya Posta itahakikisha bidhaa zao zinawasili hadi ndani ya Kiwanja cha Sabasaba salama na kwa wakati. Hii itasaidia kuwavutia zaidi washirika wa nje kuja kushiriki maonesho haya ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, na kutanua soko la kimataifa,” amesema Mbodo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis, amesema ushirikiano huo na Posta unaongeza thamani ya maonesho hayo na sasa yanakuwa ya kisasa zaidi.
“Hatutakuwa na mikokoteni ndani ya maonesho zaidi ya usafiri wa kisasa kutoka Shirika la Posta kwa gharama nafuu na kuimarisha soko la ndani na kimataifa. Pia hata wateja, wanaweza kutembelea mabanda ya biashara kwa kutumia usafiri huo wa kisasa ambao unapatikana katika ‘app’ ya za Swift Pack ambayo pia inakupa fursa ya kununua tiketi ya kuingia katika maonesho hayo,” amesema Latifa.
Amefafanua kuwa kwa washiriki wa kimataifa watapaswa kuwasiliana na Posta ili kupanga huduma ya Cargo mapema na kutoa maelezo ya mizigo kama vile kiasi, uzito na muda wa kuwasili ili kuharakisha mchakato wa usafirishaji na forodha.
Amesema hadi sasa wafanyabiashara kutoka nchi zaidi ya 19 wamethibitisha kushiriki katika maonesho ya mwaka huu ambapo wanatarajia kuwa na kampuni zaidi ya 5,000.