
Na Philipo Hassan, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha ushirikiano na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Utalii nchini iweze kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akifungua Mkutano wa Tatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi katika Utalii (Ministerial Public Private Dialogue – MPPD) uliofanyika leo Mei 13, 2025 jijini Dodoma.
“Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma, miundombinu ya utalii na utangazaji wa vivutio vya utalii.
Aidha, idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,141,895 huku mapato yatokanayo na shughuli za utalii yakifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.3” ameeleza Dkt. Balozi Chana.
Kutokana na taarifa ya World Tourism Barometer ya Januari 2023 imeitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizovunja rekodi ya idadi kubwa ya watalii wa kimataifa (best performing destinations January to December, 2024).

Halikadhalika, Tanzania imeshika nafasi ya 12 duniani kwa ongezeko la watalii, ikitanguliwa na nchi kama Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Albania, El Salvador, Colombia, Andorra, Ethiopia, Curacao, Jamhuri ya Dominican na Visiwa vya US Virgin.
Aidha, Chana ameweka bayana kuwa Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa na kupata tuzo mbalimbali za utalii kwa mwaka 2024.

Baadhi ya tuzo hizo ni pamoja na Eneo linalovutia zaidi kiutalii (Africa’s Leading Destination), Eneo linaloongoza kwa utalii wa safari duniani (World’s Leading Safari Destination), Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kuwa hifadhi bora duniani, Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika (Africa’s Leading Tourism Attraction na Bodi ya Utalii Tanzania kutajwa kuwa Bodi Bora Afrika.
Chana ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wa utalii kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya Utalii kwa maslahi mapana ya Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amefafanua kuwa malipo ya fedha za kigeni ni kwaajili ya miamala ya ndani, hivyo malipo ya kimataifa katika sekta ya utalii yataendelea kufanyika kama kawaida.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amewahakikishia wadau wa utalii kuwa hakutakuwa na tozo za ghafla katika kipindi hiki na kwamba iwapo zitahitajika baadae, wadau wa sekta ya utalii watahusishwa kikamilifu.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi ili kuvutia wawekezaji, sambamba na kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni (USD) kwa wafanyabiashara wa utalii wa kimataifa.
Pia Chambulo, aliiomba serikali kushughulikia suala la bima kwa waongoza watalii na wapagazi, pamoja na kuhakikisha mikataba ya uwekezaji inakuwa na usawa kwa wawekezaji wote nchini.

Mkutano huo ulijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Wizara, Wakuu wa Taasisi za Serikali wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Musa Nassoro Kuji, wadau wa utalii pamoja na wageni waalikwa waliojitokeza kushiriki mkutano huo.
