KAMPUNI YA AIR FRANCE -KLM YAPATA BOSI MPYA AFRIKA MASHARIKI

Na Mwandishi Wetu, Nairobi  

KAMPUNI ya Air France-KLM leo imetangaza kumteua Joris Holtus kuwa Meneja Mkuu kwa Afrika Mashariki, Kusini, Nigeria na Ghana, uteuzi ambao unaanza mara moja. 

Holtus anachukua nafasi ya Marius Van Der Ham, ambaye ameongoza eneo hilo kwa miaka mitatu iliyopita na kuchangia pakubwa kuimarika kwa uwapo na ushirikiano wa kikundi hicho katika ukanda huu.

Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika uongozi wa juu katika mabara manne, Holtus analeta ujuzi mkubwa katika mikakati ya kibiashara, huduma kwa wateja na mabadiliko ya kiutendaji. 

Anarejea barani Afrika baada ya kuhudumu kama Meneja Mkuu wa Air France-KLM kwa Afrika Kusini, ambako kwa miaka mitatu alikuwa na jukumu kamili la kibiashara, kiutendaji na kiutawala.

“Tunafuraha kubwa kumkaribisha tena Joris Holtus barani Afrika katika nafasi hii muhimu ya uongozi,” amesema Hildabeta Amiani, Meneja wa Mauzo nchini Kenya wa Air France KLM.

 “Uelewa wake wa kina kuhusu masoko mbalimbali, dhamira ya mabadiliko na mapenzi yake kwa watu vinamfanya awe chaguo bora kuendeleza ukuaji wetu katika ukanda huu unaobadilika kwa kasi.”

Katika nafasi yake ya hivi karibuni kama Makamu wa Rais wa Mipango na Maendeleo ya Mauzo, Holtus aliongoza timu ya watu 100, akibadilisha muundo wa kimataifa wa mauzo wa kampuni hiyo kwa kutumia ubunifu, teknolojia na mabadiliko ya kiutendaji ili kuongeza ufanisi.

Mafanikio muhimu katika kazi yake ni pamoja na: kuzindua mpango wa Corporate Sustainable Aviation Fuel (SAF) wa Air France-KLM, ambao ni wa kwanza wa aina yake katika sekta ya usafiri wa anga.

Kuongoza mikakati ya kufufua mashirika ya ndege kupitia mabadiliko ya kidigitali na huduma bora kwa wateja.

Kusimamia ongezeko kubwa la mapato na upanuzi wa mtandao wa safari katika Amerika ya Kusini na Karibiani kama Meneja Mkuu wa Mid-Americas & Dutch Caribbean.

Kuwezesha ubunifu katika huduma kwa wateja kama vile SkyPriority na KLM’s Meet & Seat, ambazo zimeshinda tuzo.

Holtus alizaliwa Hertogenbosch, Uholanzi na ana Shahada ya Uzamili katika Uchumi wa Biashara kutoka Vrije Universiteit Amsterdam. 

Anaongea Kiholanzi na Kiingereza kwa ufasaha na ana uzoefu wa kazi kwa lugha ya Kijerumani na Kihispania.

“Nimeheshimika kurejea katika ukanda huu katika kipindi hiki cha kusisimua kwa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika,” amesema Holtus. 

“Masoko ya Afrika Mashariki, Kusini na Magharibi yamejaa fursa na ubunifu. Natarajia kushirikiana na timu zetu na wadau ili kuboresha zaidi huduma na muunganisho wa safari.”

Holtus anachukua uongozi wa ukanda huu huku Air France–KLM ikiendelea kupanua huduma zake Afrika Mashariki.

 Hivi karibuni, Air France ilizindua safari zake za ndege kuelekea Kilimanjaro, hatua inayowezesha kuingia kwao rasmi kaskazini mwa Tanzania na kuonyesha dhamira ya kukuza mtandao wa kimataifa na kuimarisha muunganisho wa Afrika na dunia.

Wakati huohuo, KLM inatoa huduma za ndege hadi Dar es Salaam kupitia Amsterdam mara saba kwa wiki. 

Pia, KLM inahudumia Kilimanjaro mara tano kwa wiki na Zanzibar mara mbili kwa wiki, hivyo kuwapa wasafiri chaguo zaidi ndani ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *