Na Mwandishi Wetu
WAJUMBE wa Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Msasani, wamefurahishwa na utelekelezwaji wa ilani ya chama hicho na kuwaomba Watanzania kuendelea kumuamini na kumchagua tena Rais Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan kuingoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Hayo yamesemwa na wajumbe hao walipokuwa wakifanya ziara maalum mkoani Morogoro kwa kutumia usafiri wa Treni ya Mwendokasi (SGR) kutoka jijini Dar es Salaam.
Safari hiyo iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Msasani, Luca Neghest imewajumuisha wajumbe na wanachama wa CCM zaidi ya 40.
Akizungumza kabla ya kusafiri, Neghest amesema wameamua kufanya ziara hiyo maalum mkoani Morogoro ikiwa ni kuhamasisha Watanzania kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa amani na kumchagua Dkt Samia kuwa Rais na Dkt. Emmanuel, John Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza kuwa Makamu wa Rais.
“Tumeamua kusafiri kwenda Morogoro kwa njia ya SGR ambayo ni matunda ya uongozi bora wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, safari yetu ni ishara ya umoja uliotukuka wa Kata ya Msasani,” amesema Neghest na kuongeza.

“Pia safari hii ni kusheherekea jinsi gani Rais Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM na Watanzania wanafurahia maendeleo katika sekta mbalimbali.Hii safari pia ni sehemu ya kufanya utalii wa ndani kwani Morogoro kuna vivutio mbalimbali vya utalii”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msasani, Nyerere Mnyupe, amesema Kata ya Msasani inaunga mkono juhudi za dhati za serikali ya Rais Samia kuleta maendeleo chanya kwa Watanzania na kudumisha amani.
Mnyupe amesema wana-Msasani wapo bega kwa bega na Rais Mama Samia na diwani wao, Neghest ambaye ameweza kuleta maendeleo katika kata yao na wananchi wanaishi kwa kushirikiana.
“Kwa kifupi, hakuna mtu ambaye hatambui kazi kubwa ya kuleta maendeleo hapa nchini inayofanywa na Rais Samia na serikali ya CCM. Tumefarijika sana na utendaji wake na uchaguzi huo ni lazima ashinde na kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo,” amesema Mnyupe.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Makangira wa Kata ya Msasani, Daima Issa, amempongeza Rais Samia kwa uongozi bora wa kuiendeleza na kuifungua nchi kwa kuleta maendeleo chanya na kuwaomba wanawake wote kutosita kumchagua tena kwa miaka mitano.
“Hii safari ni ishara ya ushirikiano wa Kata ya Msasani na jinsi gani Diwani, Neghest anavyohimiza umoja na ushirikiano. Wana Msasani tupo kitu kimoja na ndiyo maana tunasafiri kwa njia ya SGR, haya ni matunda ya uongozi bora wa Mama Samia,” amesema Daima.