Na Sarah Moses, Dodoma.
Na Sarah Moses, Dodoma.
IMEELEZWA kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025 Wizara ya Madini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17.7 .
Hayo ameyasema leo May 2,2025 Bungeni Waziri wa Madini Anthony Mavunde wakati alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya kiasi cha Bil.224.9 .
Amesema kuwa madini hayo yaliyokamatwa yalitaifishwa na watuhumiwa 75 walifikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Amesema Wizara imeendelea kupambana na kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini nchini unaofanywa na baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wasio waaminifu katika Mikoa ya kimadini ya Geita, Ruvuma, Kahama, Mwanza, Shinyanga.
Mikoa mingine ni Kagera, Dar es salaam, Mirerani, Simiyu, Singida, Chunya, Arusha, na Lindi.
“Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kujiepusha na utoroshaji wa madini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na Taifa kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde.
Pamoja na hayo amesema kutokana na jitihada zilizofanyika kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 jumla ya zaidi ya bil. 783.8zimekusanywa na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali ikilinganishwa na zaidi ya bil.548.29 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho Mwaka wa Fedha 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 42.97.
Aidha, amesema ili kuongeza maduhuli ya Serikali, Wizara imeimarisha usimamizi na ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini,
vituo vya ununuzi wa madini na mipaka ya nchi.
Hata hivyo katika hatua nyingine Waziri Mavunde alitaja vipaumbele katika mwaka 2025/2026,amesema ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati.
” kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini; kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito,kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za madini za kina”amesema
Lakini pia kurasimisha na kuendeleza wachimbaji wadogo wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ya madini.
Mwisho.