-TMDA yashika kasi kuelimisha jamii
-Serikali yatekeleza sera za kudhibiti

Na Mary Mashina
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Kwa lengo la kulinda afya ya jamii na kwa sababu ya kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa za tumbaku ikiwa ni pamoja na magonjwa yanayohusiana na tumbaku, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ameikasimisha TMDA jukumu la kudhibiti bidhaa za tumbaku kupitia Tangazo la Serikali Na. 360 la tarehe 30 Aprili, 2021. 2.
Uvutaji holela wa Bidhaa za Tumbaku kwenye Maeneo ya Umma Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, Sura 121 imekataza uvutaji wa aina yoyote ile wa bidhaa za tumbaku kwenye maeneo ya umma ili kulinda afya ya wasiotumia bidhaa hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, anasema katazo hilo linahusisha bidhaa za tumbaku zinazotambulika kisheria ambazo ni sigara, siga, sigarusi, misokoto, shisha, kiko na tumbaku ya unga.
Anasema bidhaa za tumbaku zisizovutwa (smokeless tobacco products) haziruhusiwi kutumika katika maeneo na mazingira yoyote nchini.
“Kifungu cha 12 cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, Sura 121 kimetafsiri maeneo ya umma kama mahali ambapo inatolewa huduma ya afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwaajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii, shughuli za michezo au burudani, sehemu za huduma ya chakula, majengo ya ofisi, vyombo vya usafiri wa anga, ardhi au maji, mabanda ya maonesho, masoko, maduka makubwa na maeneo mengine yoyote yanayotumiwa na umma.
“Vilevile, katika maeneo tajwa inaelekezwa bango lenye maneno yanayosomeka ‘No Smoking’ na ‘Hairuhusiwi kuvuta sigara’ yawekwe na kuonekana bayana,” anafafanua Dkt. Fimbo.

Maeneo ya kuvutia Tumbaku
Anasema maeneo yanayoruhusiwa kuvuta bidhaa za Tumbaku Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku inawataka wamiliki wa maeneo ya umma kutenga vyumba au maeneo maalum ya kuvutia ili kuwalinda wasiotumia bidhaa za tumbaku.
Anaeleza zaidi kuwa, ujenzi na mifumo ya hewa kwenye vyumba na maeneo husika yanapaswa kuzingatia masharti ya kisheria ambayo anayataja.
Mosi kutozidisha asilimia 25 ya eneo la jumla la sakafu na kutenganishwa na eneo la umma kwa ukuta na mlango wa kuingilia wenye maneno yanayoonekana na kusomeka ‘Smoking Area’ na ‘Sehemu ya kuvutia Tumbaku’.
Dkt. Fimbo anaeleza kwa kina pia kuwa na vifaa vya mfumo wa uingizaji hewa unaoruhusu moshi kwenda nje ya jengo na kutozunguka kwenye eneo lingine lolote.
Kadhalika mfumo wa hewa utapaswa kuwekewa milango na kifaa cha milango kujifunga yenyewe baada ya kufunguliwa pamoja na feni kwa vyumba visivyo na madirisha au madirisha yanayoangalia nje na madirisha yaliyowekwa juu umbali wa mita 2.4 kutoka kwenye usawa wa sakafu ili kuruhusu moshi kuelekea juu na nje ya jengo badala ya usawa na kusambaa kwenye chumba au kuwa na vifaa vya kuelekeza moshi kutoka nje ya jengo.
Mkurugenzi huyo anasema pia urefu wa chumba cha kuvutia tumbaku unapaswa kuwa siyo chini ya mita tatu kutoka kwenye dari hadi sakafuni.
Anasema pia kuainisha tahadhari za kiafya kama ilivyoelekezwa na kuwekewa vifaa visivyohamishika na vya kupambana na moto; na kuwa na chumba kilichowekewa vifaa visivyoshika moto.
Anasema aidha, kanuni ndogo ya 7 (1) na (2) ya Kanuni za Bidhaa za Tumbaku za mwaka 2014, inawataka wamiliki wote wa majengo yanayotumiwa na watu wengi kuweka vifaa vya kubaini moshi wa tumbaku na kuweka alama zinazosomeka “This Building is installed with a smoke detector’ au ‘Jengo hili limefungwa mitambo ya kubaini moshi wa tumbaku’
Dkt. Fimbo anasema elimu hiyo wanaitoa kupitia vyombo vya habari, maonesho mbalimbali ya kimataifa kama Sabasaba, Nanenane na kuwafikia wananchi katika maeneo ya mikusanyiko mbalimbali.
“Suala la elimu ni jambo kubwa na tunaendelea nalo kwa kasi kwa kutumia njia nilizokutajia hivyo ni muhimu jamii kuamua kubadilika sasa na kuacha kutumia tumbaku hadharani,” anasema Dkt. Fimbo.

Hali ilivyo kitaifa
Kwa mwaka watu 21,800 hupoteza maisha nchini kutokana na maradhi yatokanayo na uvutaji wa tumbaku.
Licha ya takwimu hizo, serikali imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti athari zinazotokana na matumizi hayo.
Taarifa za Uwekezaji na Udhibiti wa Tumbaku nchini, zinaeleza kuwa, vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku huchangia asilimia sita ya vifo vyote vinavyotekea nchini.
Kwenye upande wa matibabu, Serikali hutumia Sh. bilioni 110 kushughulikia maradhi yatokanayo na tumbaku, huku hasara ya Sh. bilioni 337 ikipatikana kutokana na kupoteza nguvu kazi ya vijana wanaofariki kabla muda.
Licha ya elimu kuhusu kuacha matumizi ya tumbaku, serikali inaendelea kutekeleza sera mbalimbali za kudhibiti uharibifu wa mazingira unaotokana na kilimo cha tumbaku, ikiwa ni pamoja na kuhimiza teknolojia rahisi za ukaushaji wa tumbaku kwa nishati chache.
Mtaalam aeleza athari za kiafya
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Mwanaada Kilima, anasema asilimia 90 ya saratani ya mapafu na koo inatokana na matumizi ya tumbaku wakati bidhaa hizo zikichangia asilimia 40 ya aina nyingine ya saratani.
“Nimeona madhara mengi na makubwa. Matumizi ya tumbaku ya aina yoyote ile iwe ya kusokota, kumung’unya, sigara au za kielektroniki ni majanga,” anasema.
Dkt. Kilima anaeleza kuwa mbali ya saratani, mtu anapovuta sigara, ndani ya saa moja presha yake na mapigo ya moyo yanapanda kwa kasi kuleta athari kubwa kwa sababu baada ya muda, atakuwa ni mgonjwa ya shinikizo la juu la damu, mishipa ya fahamu, ubongo na hata kupata kiharusi.
Anasema moshi wa sigara unaharibu kinga asilia ya mapafu na hivyo kuyafanya kushindwa kuzuia vimelea vya maradhi yakiwamo ya kifua kikuu na mfumo wa upumuaji.
Anasema mtu anayetumia bidhaa za tumbaku katika umri mdogo, anaathirika zaidi kimwili hususani ukuaji wa ubongo ambao unakoma kukua mara tu anapoanza kutumia bidhaa hizo.
TTCF yatia neno
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutgard Kagaruki, anasema matumizi ya tumbaku yanaongezeka zaidi nchini kutokana na watengenezaji kuongeza vionjo vya ladha hasa kwenye shisha ili kuwalaghai watumiaji wasione wanavuta tumbaku.
“Kama hakuna hatua madhubuti zitakazochukuliwa, miaka mitano au 10 ijayo, kwa kiwango ambacho vijana wanavuta shisha na sigara za kielektroniki, Ocean Road, Muhimbili na hospitali nyingine kwenye kliniki za kisukari hakutatosha. Tuna vijana ambao wanaelekea kupata uraibu kutokana na matumizi holela ya shisha. Tuna janga kubwa, tunaiomba serikali ichuke hatua,” anasema Dkt. Kagaruki.
Wananchi waeleza hali ilivyo

Jumanne Kashisha mkazi wa Ilala, yeye havuti tumbaku, lakini anaishi na kukutana na wanaovuta tumbaku hususani sigara, ambapo anasema kwasasa elimu imeendelea kusaidia watu kupunguza kuvuta mbele za watu.
“Saivi kiukweli watu hawavuti hadharani kama zamani, utamjua huyu anavuta kwa harufu yake. Ni wachache sana ambao hawana haya kuvuta hadharani. Nashauri elimu iendelee kutolewa ili kusaidia wasiovuta wasivutishwe,” anasisitiza.
Naye dereva wa daladala ya Bugurugu Gongo la Mboto anasema, anavuta lakini akifika mwisho wa kituo wakati akisubiri kupakia abiria anajitenga pembeni, akimaliza anaingia kwenye gari.
“Kama tukitengewa maeneo ya kuvutia hasa kwenye maeneo ya mikusanyiko kama vituo vya daladala itasaidia hata huo moshi kidogo wanaopata wenzetu hawataupata na kuondoa athari zaidi,” anasema.
Siku ya Kuzuia Tumbaku Duniani huadhimishwa Mei 31 kila mwaka na kaulimbiu ya mwaka huu, “Kulinda Watoto dhidi ya Kuingiliwa na Sekta ya Tumbaku,” inaangazia haja ya haraka ya kuweka hatua madhubuti ili kukilinda kizazi chetu cha vijana dhidi ya mbinu za ujanja zinazotumiwa na kampuni za tumbaku.
