
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Kimei ametajwa kuwa kinara wa kuzungumzia mahitaji ya wananchi kwa kuwa miongoni mwa wabunge vinara wa kusema, kuchangia au kuhoji katika kila kikao cha bunge la 12 linalotarajiwa kuvunjwa mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge la Tanzania inaonyesha Dk.Kimei amechangia mara 49 na kuuliza maswali 110 yanayohusu jimboni na yanayogusa Taifa kwa ujumla.
Mbunge huyo ni aina ya viongozi wanaoipenda kazi yao na kuguswa ambao wamekuwa wakioonekana katika majimbo yao wakifanya mikutano ya wananchi kutoa mrejesho, kusikiliza na kutatua kero pamoja na ziara za ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Akiwa bungeni Dkt. Kimei ameuliza kwa vile Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) linalenga watu wa chini, Je, wana mpango gani wa kuiongezea SIDO uwezo wa kujitangaza na kutekeleza maonesho kwenye miji midogo midogo kama Mji wa Himo?.
Dkt. Kimei pia amehoji, utaratibu gani utumike kuhusisha vijana wanaoishi jirani la Mlima Kilimanjaro ili kunufaika na ajira zinazotolewa.

“Zaidi ni kwamba hawa operators wanakuja na watu kutoka sehemu nyingine ambao hawajui hii mikataba. Kwa hiyo, hawaajiri wale vijana ambao wanatoka kwenye vijiji karibu na ule mlima, wao hawaelewi mikataba hiyo hivyo wanalipwa kidogo sana.
“Je, hatuwezi kuweka uwiano fulani hasa kwa zile shughuli ambazo hazihitaji taaluma kwamba hawa operators waweze kuajiri au kuchukua vijana kutoka kwenye kundi la wale ambao wanatoka karibu na mlima kwa sababu hiyo ni njia mojawapo ya kuwapa motosha?” amehoji Dkt. Kimei.


