
Na Mwandishi Wetu, Mara
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko leo Aprili 16,2025 ameongoza maelfu ya wananchi pamoja na viongozi mbalimbali kwenye shughuli ya maziko ya aliyekua Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Gissima Nyamo-Hanga, yaliyofanyika katika eneo la Migungani wilayani Bunda mkoani Mara.
Akizungumza mara baada ya ibada ya mazishi Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko, amemuelezea marehemu Mhandisi Gissima kuwa ameacha urithi mkubwa wa muunganiko ndani ya TANESCO wenye lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wakati wote.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimuamini kutokana na uwajibikaji wake hivyo ametuma salamu za pole kwa familia, Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO ambapo amefafanua kuwa ameacha alama kubwa hasa katika kuhakikisha miradi ya umeme inakamilika kwa wakati na Watanzania wananufaika na nishati hiyo muhimu.

“Mhandisi Gissima ni hazina ya mipango, baada ya nchi kuzalisha umeme wa kutosha marehemu ameongoza majadiliano na nchi ya Zambia ambayo hivi karibuni tutaanza kuwauzia umeme kutokana na msukumo mkubwa alioufanya. Hakika historia itaandikwa na tutaendelea kuyaenzi yote aliyoyaacha,’’amesisitiza Dkt. Biteko
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TANESCO Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema licha ya utendaji mahiri uliooneshwa na marehemu Mha. Gissima enzi za uhai wake lakini shukrani za pekee ni kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa maono yake alimuona anafaa na kumteua katika kipindi kigumu cha upungufu wa umeme nchini.
“Nitoe pole sana kwa familia kwa kuwa imepata pigo lakini kutokana na mema aliyoyafanya wakati wa uhai wake ni faraja kubwa.Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuona marehemu Mha. Gissima anafaa ndani ya Shirika na hakika kazi yake ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika imeonekana, ’’ameeleza Dkt. Nyansaho
Mhandisi Gissima alijiunga na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO baada ya kuteuliwa na Rais Septemba 22 mwaka 2023 lakini kabla ya hapo amewahi kufanya kazi katika kampuni ya BP Tanzania, Business Care Services na ESD LTD Nchini Uingereza, Wakala wa Umeme Vijijini REA na Wakala wa majengo TBA.




