Tamisemi yaomba Tril. 11.78/- bajeti ya 2025/26

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imewasilisha bungeni makadirio ya mapato kwa mwaka 2025/26 yenye takribani Sh. trilioni 11. 783 kwaajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh. trilioni 10.125 zilizotengwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Sh. trilioni 11.783 na kuwa na ongezeko la zaidi ya Sh. trilioni 1.66. Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, amesema Sh. trilioni 3.95 zinaombwa kwaajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Sh. trilioni 2.5 ni fedha za ndani, ikijumuisha Sh. bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri na Sh. trilioni 1.45 ni fedha za nje.Pia amesema Sh. trilioni 7.84 ni kwaajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Sh. trilioni 6.3 na matumizi mengineyo Sh. trilioni 1.53 ikijumuisha Sh. trilioni 1. 067 za mapato ya ndani ya halmashauri.

“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. Tamisemi haitafuti sifa ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida.”Aidha, Mchengerwa ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana, kusonga mbele kwa mshikamano.“Kwa dhamira hiinna kwa imani kubwa katika maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”“Kwa hiyo, tunasema kwa ujasiri mkubwa, Tamisemi ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Kila Shilingi ina jukumu, kila kiongozi ana wajibu na kila mwananchi ana nafasi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *