Ujenzi wa barabara za lami waongezeka kwa 71%, 2024/25

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa urefu wa barabara za Vijijini na Mijini zilizojengwa kwa kiwango cha lami umeongezeka kutoka Kilomita 2,025 hadi Kilomita 3,467.30 sawa na asilimia 71.22.

Hayo ameyasema leo Aprili 16, 2025 wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26 Bungeni, jijini Dodoma.

Kwa upande wa ujenzi wa barabara za changarawe, Mchengerwa amesema kuwa umeongezeka kutoka Kilomita 24,493 hadi Kilomita 44,372.21 sawa na asilimia 81.16 na kuongeza mtandao wa barabara kutoka Kilomita 108,946.19 hadi Kilomita 144,429.77 sawa na asilimia 32.57.

Kuhusu matumizi ya teknolojia mbadala katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, Mchengerwa amelieza bunge kuwa barabara zenye urefu wa kilomita 61.7 zinaendelea kufanyiwa tafiti Ili kupunguza gharama za ujenzi, matengenezo na ukarabati.

“Tulipotoka kulikuwa na vumbi, lakini leo tunatembea kwenye lami. Tulipotoka kulikuwa na miteremko isiyopitika, leo tuna barabara zinazounganisha ndoto na fursa.

Kuongezeka Kwa barabara za changarawe kwa asilimia 81.16 na lami kwa asilimia 71.22 ni ushahidi wa nchi inayojenga msingi wa maendeleo kwa kila mtanzania, kuanzia kijijini hadi mjini. Huu sio mradi wa barabara tu, huu ni mradi wa matumaini” amefafanua Chengerwa.

Mchengerwa amebainisha kuwa kila Kilomita moja ya barabara ni daraja kati ya umasikini na maendeleo na kuongeza kuwa ni njia ya mtoto kufika shuleni, mama kufika hospitali, mkulima kupeleka mazao sokoni na taifa kusonga mbele.

Kwa mujibu wa Mchengerwa kuongeza mtandao wa barabara kutoka kilomita 108,946 hadi zaidi ya kilomita 144,000 si takwimu tu ni mabadiliko ya kweli yanayoonekana, yanayogusika na yanayogusa maisha.

“Barabara hizi ni sauti ya Serikali inayosema: ‘Hatukuwaacha nyuma. Hizi ni njia zinazotufikisha kwenye Tanzania ya viwanda, fursa na mshikamano” ameongeza Mchengerwa.

Katika bajeti ya Mwaka wa fedha 2024/25 Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA iliidhinishiwa Sh. bilioni 908.16 kwaajili ya ujenzi, ukarabati, matengenezo ya barabara na hadi mwezi Machi, 2025 Sh. bilioni 468.40 zimetolewa sawa na asilimia 55.68 ya fedha zilizoidhinishwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *