Na BBC
“NISAIDIE, ninateswa na mwajiri wangu,” Meriance Kabu aliandika. “Ninatapakaa damu kila siku, nisaidie!”
Kisha akaikunja ile karatasi kwa haraka na kuitupa nje ya milango ya chuma iliyofungwa ya ghorofa katika viunga vya Kuala Lumpur ambako alikuwa akifanya kazi kama kijakazi.
Mwanamke aliyekuwa akipita akaiokota. Mara tu alipoisoma, mara moja aliipeleka kwa afisa wa polisi aliyestaafu ambaye aliishi katika nyumba zilezile. “Ikiwa angebaki huko, bila shaka angekufa,” alisema baadaye.
Siku hiyo hiyo, tarehe 20 Desemba 2014, polisi wa Malaysia walibisha mlango wa ghorofa aliyokuwa akiishi Meriance. Alikuwa hajatoka nje kwa miezi minane.
“Nilihisi kama ninaanguka,” anasema, akikumbuka wakati alipowaona maafisa. “Walisema, ‘Usiogope, tuko hapa’. Wakati huo nilihisi nguvu tena. Nilihisi kama ninaweza kupumua tena. Maafisa waliniita karibu na nikawaambia ukweli.”
Miaka tisa imepita, Meriance bado anapigania haki. Kesi yake, ambayo sio ya kipekee, inafichua jinsi wafanyikazi wahamiaji wasio na hati walivyo hatarini na ni mara ngapi haki huwakwepa hata wale ambao wamethubutu kusimulia hadithi zao.
Mnamo 2015, polisi walimshtaki mwajiri wa Meriance, Ong Su Ping Serene, kwa kusababisha maumivu makali, jaribio la mauaji, biashara ya binadamu na ukiukaji wa uhamiaji. Alikana makosa.
Meriance alitoa ushahidi wake mahakamani kabla ya kurejea nyumbani kwa familia yake. Miaka miwili baadaye alipata habari kutoka kwa ubalozi wa Indonesia kwamba waendesha mashtaka walikuwa wamefuta kesi hiyo kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
“Mwajiri alikwepa mkono wa sheria, haki iko wapi?” anauliza balozi wa nchi hiyo nchini Malaysia, Hermono ambaye alikutana na Meriance mwezi Oktoba.
Ubalozi huo umemkodishia mshauri wa kisheria na umekuwa ukishawishi kesi dhidi ya mwajiri wa Meriance ianze tena.
“Sababu ya kuchelewa ilikuwa nini? Je, muda wa miaka mitano hautoshi? Tusipoendelea kuuliza, itasahaulika, hasa kwa vile Meriance tayari amerejea nyumbani.”
Haijulikani ni kwa nini kesi chache za unyanyasaji huishia kwa mwendesha mashtaka nchini Malaysia lakini wanaharakati wanalaumu utamaduni unaowaona wafanyakazi wa nyumbani, ambao wengi wao ni Waindonesia, kama raia wa daraja la pili wasiostahili ulinzi sawa na Wamalaysia.
Wizara ya mashauri ya kigeni ya Malaysia iliambia BBC “watahakikisha kwamba haki itapatikana kwa mujibu wa sheria”.
Mnamo mwaka wa 2018 mahakama ya Indonesia iliwafunga jela wanaume wawili kwa kosa la kusafirisha Meriance. Hakimu aliamua kwamba alikuwa ametumwa kufanya kazi nchini Malaysia “kama mjakazi wa Ong Su Ping Serene ambaye alimtesa, na kusababisha majeraha mabaya” ambayo yalisababisha alazwe hospitalini.
Kisa cha Meriance kilielezewa kwa kina katika hukumu hiyo, ambayo ilisema mwajiri alimpiga sana, kumvunja pua katika tukio moja, na mara nyingi alikuwa akimtesa kwa pasi ya moto, kibano, nyundo, fimbo na koleo.
Miaka minane baadaye, mwili wake bado una alama za mateso haya. Kuna kovu kubwa kwenye mdomo wake wa juu, meno yake manne hayapo na sikio moja limeharibika.
Mumewe Karvius alisema hakuweza kumtambua baada ya kuokolewa: “Nilishtuka sana waliponionyesha picha za Meri akiwa hospitalini.”
Mwaka jana, Malaysia na Indonesia zilitia saini makubaliano ya kuboresha hali ya wafanyakazi wa nyumbani wa Indonesia nchini humo. Indonesia sasa inashawishi kesi dhidi ya mwajiri wa Meriance irejelewe.
Wafanyakazi wasio na hati kama yeye wako katika hatari zaidi kwa sababu hati zao za kusafiria huchukuliwa na wanaishi na mwajiri katika nchi ya kigeni, hivyo kuwaachia chaguo kidogo kutafuta usaidizi.
“Kila mtu anahitaji kuwajibika zaidi,” anasema Mbunge wa Malaysia Hannah Yeoh ambaye anataka kuona mwisho wa kile anachoelezea kama utamaduni wa ukimya nchini kuhusu unyanyasaji wa wafanyikazi wa nyumbani.
Wizara ya nguvu kazi ya Malaysia inasema kuna zaidi ya wasaidizi wa nyumbani 63,000 wa Indonesia katika nchi yao, lakini hiyo haijumuishi wafanyikazi wasio na vibali. Hakuna makadirio ya wazi juu ya idadi yao. Ubalozi wa Indonesia unasema kuwa umepokea ripoti za karibu kesi 500 za unyanyasaji katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Idadi hiyo ni sehemu ndogo sana, anasema Balozi Hermono, kwa sababu kesi nyingi, haswa zile zinazohusisha wafanyikazi wasio na hati, bado haziripotiwi.
“Sijui ni lini hii itaisha. Tunachojua ni kwamba kuna wahasiriwa zaidi na zaidi – kuanzia kwa mateso, kutolipwa mishahara na uhalifu mwingine.”
Ubalozi haujafuatilia ni kesi ngapi za unyanyasaji zimesababisha kufunguliwa mashtaka. Lakini kumekuwa na maamuzi ya hali ya juu. Mwaka wa 2008 mwanamke wa Malaysia alihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela kwa kumtesa mjakazi wake raia wa Indonesia. Miaka sita baadaye wanandoa walihukumiwa kifo kwa kumuua mfanyakazi wao wa nyumbani Muindonesia.
‘Nitapigana hadi nife’
“Nitapigania haki hadi nife,” Meriance anasema. “Ninataka tu kuuliza mwajiri wangu wa zamani, ‘Kwa nini ulinitesa?’
Alikuwa na umri wa miaka 32 alipoamua kutafuta kazi nje ya nchi ili “watoto wasililie tena chakula”. Maisha yalikuwa magumu katika kijiji chao huko Timor Magharibi, ambako hakuna umeme au maji safi ya bomba. Na mshahara wa mume wake kama kibarua haukutosha kutunza familia yao ya watu sita.
Alichukua ofa ya kazi huko Malaysia na alitamani kujenga nyumba kwa familia yake.
Alipofika Kuala Lumpur mnamo Aprili 2014, wakala alichukua pasipoti yake na kuikabidhi kwa mwajiri wake. Waajiri nchini Indonesia walikuwa tayari wamechukua simu yake.
Lakini Meriance alikuwa na matumaini ya maisha bora. Kazi yake ilikuwa “kumtunza bibi”, mama wa mwajiri wake Serene, ambaye alikuwa na umri wa miaka 93 wakati huo.
Wiki tatu baada ya kuanza kazi yake, anasema, vipigo vilianza.
Jioni moja, Serene alitaka kupika samaki lakini hakuweza kuipata kwenye jokofu kwa sababu Meriance alikuwa ameiweka kwenye friji kimakosa. Ghafla, Meriance anasema alipigwa kwa samaki aliogandishwa. Kichwa chake kilianza kuvuja damu.
Baada ya hapo, anasema, alipigwa kila siku.
Anasema kamwe hakuruhusiwa kuondoka kwenye ghorofa. Lango la chuma la ghorofa lilikuwa limefungwa kila wakati na hakuwa na ufunguo. Majirani wanne waliokuwa wakiishi mtaa mmoja hawakujua kuwepo kwake hadi siku polisi walipofika.
“Nilimwona tu usiku ambao aliokolewa,” mmoja wao alisema.
Meriance anasema mateso na vipigo vilikoma pale tu mwajiri wake alipochoka. Kisha akamuamuru Meriance asafishe damu yake iliyokuwa imetapakaa sakafuni na kuta.
Anasema, kuna nyakati ambapo alifikiria kujikatilia mbali maisha yake, lakini mawazo ya watoto wake wanne kule nyumbani yalimfanya aendelee.
“Pia nilifikiria kupigana,” alisema. “Lakini kama ningepigana, ningekufa.”
Kisha siku moja – mwishoni mwa 2014 – alijitazama kwenye kioo na akahisi kitu kinabadilika: “Sikuweza kuvumilia zaidi. Nilikuwa na hasira, si kwa mwajiri. Nilijichukia mwenyewe. Ilinibidi kuthubutu kujaribu kutoka.”
Hapo ndipo alipoandika barua ambayo ingemkomboa.
BBC ilifanya majaribio mengi ya kumtafuta mwajiri wake Ong Su Ping Serene kwa majibu yake kwa madai hayo, lakini alikataa kufanya hivyo.
Meriance anasema kupigania kwake haki pia ni kwa niaba ya wengine kama yeye – na wale ambao hawakufanikiwa.
Balozi Hermono anashughulikia kesi nyingine ya mfanyakazi wa ndani ambaye anasema aliteswa “bila sababu za kibinadamu” na njaa. Alikuwa na uzani wa kilo 30 tu alipookolewa. Mwajiri wake yuko kwenye kesi kwa sasa.
Lakini kuna wale kama Adelina Sau mwenye umri wa miaka 20 ambao hawakuokolewa kwa wakati. Inadaiwa alikufa kwa njaa na kuteswa na mwajiri wake, jambo lililosababisha kifo chake.
Mwajiri wake alishtakiwa kwa mauaji lakini mwaka wa 2019 upande wa mashtaka uliondoa mashtaka. Rufaa ya kufunguliwa tena kwa kesi hiyo ilikataliwa mwaka jana.
Adelina alitoka wilaya moja na Meriance huko Timor Magharibi.
Meriance anasema alikutana na mama Adelina kijijini kwao na kumwambia, “Ingawa binti yako amekufa sauti yake iko ndani yangu.”