Na Bdrudin Yahaya
KIUNGO wa timu ya Singida Black Stars, Kelvin Nashon, huenda akakamilisha dili la kujiunga na Yanga kwa usajili wa mkopo katika dirisha la usajili mdogo ambalo linatarajia kufunguliwa wiki ijayo.
Mazungumzo baina ya pande mbili yanatajwa katika hatua nzuri na mara tu baada ya usajili kufunguliwa mchezaji huyo anaweza kutambulishwa.
Yanga SC inahitaji mchezaji wa nafasi ya kiungo ambaye anaweza kuwasaidia Khalid Aucho na Mudathir Yahaya ambao wanaonekana kutokuwa na muda wa kupumzika.
Mwanzo wa msimu huu, timu hiyo imemsajili Aziz Andabwile ambaye baadaye aliyekuwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alimfanya kuwa beki wa kati kwa ajili ya kuwasaidia Bakari Nondo, Ibrahim Bacca na Dickson Job.
Pia Yanga ilijaribu kumsajili Yusuph Kagoma ambaye baadaye aliibukia Simba ambaye anacheza hadi sasa kwenye msimu huu.
Habari za kuaminika zinadai usajili wa Nashon hauna maana kuwa Yanga wanataka kuacha mpango wa kuleta kiungo wa kimataifa ambaye atakuja kuziba pengo la Aucho mwisho wa msimu.