Kocha Yanga SC aing’arisha FC Lupopo Ligi Kuu DRC

Na Mwandishi Wetu

KOCHA wa zamani wa timu ya Yanga SC, raia wa Ubelgiji, Luc Eymael amekuwa na wakati mzuri baada ya timu yake ya FC Lupopo kutembeza vichapo katika Ligi Kuu ya DR Congo.

Eymael amejiunga na klabu hiyo msimu huu ambapo amevuna ushindi katika mechi tatu mfululizo.

Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Tshinkuku ambapo Lupopo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kabla ya kuichapa TP Mazembe bao 1-0.

Mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Simba ambayo ilivunjika kutokana na vurugu za mashabiki ambazo zilitokea uwanjani.

Licha ya vurugu za hapa na pale ambazo zilizotokea katika mchezo huo lakini Kocha Eymael ameendelea kuonesha ubora wa kikosi chake na kushinda tena mabao 2-0 dhidi ya Lubumbashi.

Mchezo unaofuata unatarajiwa kuchezwa kesho dhidi ya Tanganyika.

Akizungumza na mtandao wa Tanzania Leo kutoka DR Congo, Eymael amesema anashukuru Mungu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kumpa matokeo mazuri.

Kocha Eymael, akitoa maelekezo kwa wachezaji wake

Amesema kazi yake kubwa ni kuhakisha anafanya kazi kwa weledi na kutengeneza kikosi Bora ambacho kitazidi kutoa matokeo mazuri kwa timu yake.

“Nafarijika kuona timu yangu imekuwa na matokeo mazuri tangu nimejiunga, kazi ya mpira inahitaji akili na weledi lakini pia kuwa na mipango kwa kile unachofanya,” amesema Eymael.

Mbali na hayo, Kocha Eymael amesema hivi karibuni kulitokea sintofahamu akiwa katika maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Simba, ambapo kijana aliyejitambulisha kama Mwandishi wa Habari alisababishia vurugu uwanjani.

Amesema suala hilo lilifika mbali zaidi na kuchapishwa katika mtandao wa kijamii wa Gulilit koba ambapo imedaiwa kutoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya timu hiyo kabla ya mazoezi ya klabu hiyo.

Amesema madai haya yalikuwa mazito kiasi kwamba yalizua uchunguzi wa kina ndani na nje ya klabu ili kujua zaidi na madai hayo ni sambamba na yale yaliyotangulia kutolewa wiki mbili zilizopita.

Aidha amewashutumu TP Mazembe wamekuwa wakijaribu kuwavuruga kila wakati kutokana na ushindani mkubwa baina yao.

“Ushindani kati ya Mazembe na sisi ni mkubwa sana kiasi kwamba kila siku wanajaribu kitu, wachezaji wangu walirekodi kila kitu kilichotokea pale uwanjani na yule jamaa alinisukuma na kunirushia chupa ya maji lakini namshukuru Mungu kwamba sikujibu mashambulizi na sikuguswa kabisa na vitisho vyake vya kifo,” amesema Eymael.

Hata hivyo uongozi wa Klabu ya FC Lupopo umetoa taarifa rasmi kuwa Kocha Eymael hana kosa na hajatamka lolote kuhusu masuala ya ubaguzi wa rangi bali tukio hilo lilikuwa kama hujuma wa kuharibu mchezo.

Katika hatua nyingine uongozi huo, umemchukulia hatua kijana huyo ili kutoa maelezo ya kwanini alivamia uwanjani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *