Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya waogeleaji saba, wamevunja rekodi katika mashindano ya High Performance Training (HPT) Mixed na Open Swimming, yaliyomalizika mwishoni mwa wiki katika bwawa la kuogelea la International School of Tanganyika (IST) Masaki, jijini.
Mashindano hayo yalishirikisha zaidi ya waogeleaji 150, yaliandaliwa kwa lengo la kuwapima uwezo waogeleaji kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Katika mashindano hayo, waogeleaji wawili wameng’ara zaidi kwa kuvunja rekodi mbili za HPT kila mmoja na kuzawadiwa sh. milioni 1 kutoka kwa waandaaji katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Pepsi, International School of Tanganyika (IST), JD Events na City Ambulance.
Muogeleaji Nicolene Viljoen (12) wa Klabu ya Riptides, amevunja rekodi ya meta 200 Individual Medley, akitumia muda wa 2.34.90 na kuvunja rekodi ya awali ya 2.44.76.
Nicolene pia amevunja rekodi ya mita 100 Breaststroke, akimaliza kwa muda wa 1.21.33 na kufuata rekodi ya awali ya 1.25.83.
Pia Phares Mteki (8) wa klabu ya Ziwa Victoria, amevunja rekodi mbili. Phares aliweka rekodi mpya katika mita 50 freestyle kwa muda wa 34.11, akipiku rekodi ya awali ya 35.42.
Pia amevunja rekodi ya mita 50 butterfly, akimaliza kwa 39.52 na kuvunja rekodi ya awali ya 43.71.
Waogeleaji ambao wamezawadiwa sh. 500,000 kwa kuvunja rekodi moja ni pamoja na Heydleen Kagashi (11) kutoka Taliss-IST swimming Club, aliyeboresha rekodi ya mita 100 freestyle kwa muda wa 1.09.13, akipiku rekodi ya awali ya 1.21.33.
Pia Aryiel Angemi (12) kutoka Taliss-IST, amevunja rekodi ya mita 50 freestyle, akitimka kwa 28.31 na kuvunja rekodi ya awali ya 38.38.
Muogeleaji wa Dar es Salaam Swimming Club (DSC), Konhelli Mhella (9), ameweka rekodi mpya ya mita 50 freestyle kwa muda wa 32.89, akipiku rekodi ya awali ya 32.90.
Mwingine kutoka Dar Swim Club, Austin Okore (15), ameweka muda mpya wa 31.45 na kuvunja rekodi ya awali ya 31.98.
Pia Mina Siebert (10) kutoka HPT ameweka muda mpya wa 24.63 katika mita 100 butterfly, akipiku rekodi ya awali ya 28.71.
Kwa mujibu wa Meneja wa HPT, Francisca Binamungu, amewapongeza waogeleaji wote, makocha, viongozi, na wadau kwa mafanikio ya mashindano hayo.
“Tumefikia lengo letu kwani waogeleaji wengi wametengeneza muda mpya wa kuogelea (PBs) huku wengine wakivunja rekodi.
Kwa upande wa Kocha wa timu ya Taifa ya Kuogelea ya Tanzania, Alexander Mwaipasi, alionyesha kuridhishwa na maendeleo ya waogeleaji hao, akisema:”Nimevutiwa na viwango vilivyoonyeshwa na waogeleaji. Tuko kwenye mwelekeo mzuri na naamini watafanikiwa katika mashindano ya kimataifa yajayo. Hili ndilo lengo kuu la HPT.”