EU: Samia shujaa wa maendeleo

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

UMOJA wa Ulaya (EU), umesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayefanya mapinduzi makubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini kwenye kipindi kifupi cha uongozi wake madarakani.

Kwa mujibu wa umoja huo, tangu Rais Dkt. Samia aingie madarakani Machi 19, 2021, uchumi wa Tanzania unakuwa kwa haraka, kuchochea uwekezaji, biashara baina ya Tanzania na EU.

Waziri wa Biashara za Kimataifa, Uchumi wa Ufaransa, Olivier Becht, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la  Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na EU.

Alisema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na EU ni wenye tija katika uwekezaji.

Alieleza kuwa, Tanzania ni lango la nchi zaidi ya sita zisizo na bahari yenye utulivu wa kisiasa, mageuzi ya kidemokrasia ndani ya muda mfupi wa miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.

“Uongozi wa Rais Dkt. Samia unasifika katika jumuiya za kimataifa na sekta binafsi, serikali yake inaonesha utayari wa kuondoa vikwazo mbalimbali,” alisema.

Becht aliongeza kuwa, ipo haja ya kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa biashara, uwekezaji kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka umoja huo.

Jukwaa hilo limeshirikisha zaidi ya washiriki 800 kutoka mataifa 27 ya Umoja huo, kampuni 150 za kitanzania likiwa na kauli mbiu isemayo; “Changamkia  Fursa za Uwekezaji Tanzania ambazo hazijatumika”

Mapinduzi makubwa ya maendeleo ambayo Rais Dkt. Samia anaendelea kuyafanya nchini ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo kwenye sekta mbalimbali nchini.

Sekta hizo ni pamoja na elimu, afya, kilimo, barabara, maji, nishati ya umeme, kutekeleza miradi ya kimkakati ili kuchochea ukuaji uchumi, maendeleo ya wananchi.

Kwa kutambua kilimo ndicho kinachoajiri asilimia 60 ya Watanzania, Serikali ya Awamu ya Sita ilitenga sh. bilioni 150 kwa ajili ya pembejeo za ruzuku.

Usambazaji wa pembejeo hizo unaendelea nchi nzima  kwenye baadhi ya mikoa mbolea ikiuzwa kwa nusu ya bei ya mwaka 2021 kati ya sh. 40,000 na sh. 70,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.

Mwaka 2021, mbolea ziliuzwa zaidi ya sh. 150,000 kwa mfuko mmoja, hivi sasa, mbolea ya ruzuku imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wote nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imesajili wazalishaji mbolea watatu, wasambazaji 31, mawakala 3,103 katika mikoa yote nchini.

Wakulima waliosajili kwa ajili ya kupata mbolea ni 3,264,440, kupitia mfumo wetu wa kidigitali wakulima waliosajiliwa ni 2,793,469.

Hadi kufikia Januari 9, 2023 mbolea ya ruzuku tani 194,259 yenye thamani ya sh. bilioni 208.6 ilisambazwa kwa wakulima 560,451 sawa na asilimia 20 ya wakulima waliosajiliwa nchi nzima.

Akizungumza na Tanzania Leo katika mahojiano maalum, Msemaji Mkuu wa Setikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Gerson Msigwa, alisema Rais Dkt. Samia ameweka historia katika sekta hiyo nchini.

Alisema Rais Dkt. Samia ameongeza bajeti ya kilimo kutoka sh. bilioni 254 hadi bilioni 954 jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.

“Hii yote ni dhamira njema ya Rais wetu aliyeamua kuwagusa Watanzania wote kupitia kilimo pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

“Rais Samia anaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ujenzi wake unagharimu fedha nyingi lakini kutokana na umuhimu wake inaendelea vizuri,” alieleza.

MRADI WA SGR

Msigwa alisema, miradi inayotekelezwa na Rais Dkt. Samia ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) Awamu ya kwanza kilometa 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza.

Kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam-Morogoro (km300) kinamaliziwa, kazi imefikia asilimia 99.77, Kipande cha pili, Morogoro-Makutupora  (km422) kimefikia asilimia 91.79.

Kipande cha tatu, Makutupora-Tabora (km368), kimefikia asilimia 3.95, Kipande cha nne, Tabora-Isaka  (km165) kipo asilimia 0.66.

“Januari 18, 2023 Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amewe ka jiwe la msingi ujenzi wa kipande cha tano, mkoani Shinyanga.

“Kipande hicho ni Isaka-Mwanza (km341) ujenzi wake unaendelea, umefikia asilimia 22.71, lengo la serikali ni kuiunganisha reli hiyo na nchi jirani za Rwanda, Kongo DRC, Burundi na Uganda ambako wanaitegemea Bandari ya Dar es Salaam.

Msigwa alisema, mradi huo ni mkubwa, utainufaisha Tanzania kwa mapato makubwa ya bandari, usafirishaji na ajira, kufungua biashara ya eneo la Maziwa Makuu na hivyo kuboresha maisha ya wananchi.

Kuhusu ununuzi wa mabehewa, alisema tayari mabehewa 14 mapya yaliyotengenezwa Korea Kusini yamewasili nchini, yanasubiriwa mabehewa 45 ambayo yamebaki kati ya mabehewa yote 59 ambayo Serikali imenunua kwa ajili ya mradi wa SGR. 

“Tuna vichwa 17 vya treni za umeme, seti za treni aina EMU (Electric Multiple Units) 10 ambavyo vinaendelea kutengenezwa Korea Kusini na kampuni ya Hyundai Rotem, sh. bilioni 680 zimetumika.

“Vichwa hivyo vya treni vitaanza kuingia Juni, 2023, pia tumeagiza mabehewa ya mizigo 1,430 ​Mkataba umesainiwa Februari 8, 2022 na kampuni ya CRRC International kutoka China wa sh. bilioni 292.

“Kwa sasa Shirika la Reli limekamilisha kuunganisha reli ya kisasa-SGR njia kuu kipande cha Dar es Salaam -Morogoro (km300), Morogoro -Makutupora (km422), wanaendelea na majaribio ya mifumo ya mifumo ya umeme na mawasiliano,” aliongeza.

BWAWA LA NYERERE

Akizungumzia ujenzi wa Bwawa la Nyerere katika Mto Rufiji, Msigwa alisema litaszalisha megawati 2,115 za umeme na mradi huo unaendelea vizuri.

Alisema Rais Dkt. Samia ameruhusu maji yaanze kujaa katika bwawa ikiwa ni maandalizi ya kuanza uzalishaji wa umeme ambapo mvua zinazonyesha, zinaendelea kujaza maji katika Bwawa hilo.

Msigwa alieleza kuwa, ifikapo Juni, 2024 tutaanza kupata umeme kutoka Bwawa la Nyerere ambapo hivi sasa, ujenzi wa vituo vya kupooza umeme na njia za kusafirisha umeme unaendelea.

UWANJA WA MSALATO

Akizungumzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Msigwa alisema kazi za ujenzi wa uwanja huo ilianza Aprili, 2022 na inaendelea vizuri.

Hadi sasa, Mkandaraso amefikia asilimia 10.29 ya ujenzi, awamu ya kwanza itagharimu sh. bilioni 165.6 na Serikali amewalipa fidia wananchi sh. bilioni 14.6 kati ya sh. bilioni 20.4 zilizopangwa.

“Mambo yakienda kama ilivyopangwa awamu ya kwanza itakamilika mwaka 2025/26,” alisema.

DARAJA LA JP MAGUFULU

Kuhusu Daraja na JP Magufuli, linalounganisha Kigogo-Busisi katika Ziwa Victoria, ujenzi wake unaendelea vizuri.

Hadi sasa umefikia asilimia 63, kazi ya usimikaji nguzo  za msingi umefikia asilimia 85.11, nguzo 686 kati ya nguzo zote 804 zimejengwa. 

Kuna nguzo 32 kati ya 67 zimeshajengwa sawa na asilimia 47.7, pia kuna usimikaji wa beams ambapo 208 kati ya beams 806 tayari zimewekwa.

Msigwa alisema, tayari Mkandarasi ameshalipwa sh. bilioni 315 zikiwa ni kati ya gharama za mradi mzima ambazo ni sh. bilioni 699, mradi huo umezalisha ajira 1,024, kati ya hizo, ajira 961 wamepata Watanzania.

MIRADI YA BARABARA

Msigwa alisema, serikali inaendelea kutekeleza miradi mipya ya barabara mbalimbali nchini.

Miradi hiyo inatekelezwa kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) zikiwemo za lami, changarawe, barabara za udongo na madaraja.

Hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alishuhudia utiaji saini ujenzi wa barabara muhimu na za kimkakati.

Barabara hizo ni Kajunjumele-Itungi Port mkoani Mbeya ambayo ujenzi wake utagharimu sh. bilioni 38.4, barabara ya Kitulo-Iniho kilometa 36.3 (Makete-Mbeya) na ujenzi wa mzani wa Igagala.

Mradi huo utagharimu sh. bilioni 69.8, barabara ya Kibondo-Mabamba kilometa 47.9 ambao utagharimu sh. bilioni 63.6 ambapo miradi hii yote inatarajiwa kukamilika kati ya mwaka 2025 na 2026.

Pia Serikali imesaini mkataba wa ukarabati viwanja vya ndege vya Kigoma, Tabora, Shinyanga na Sumbawanga kwa gharama ya sh. bilioni 46.7, ambao unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2024.

Viwanja hivyo ni sehemu ya mradi wa viwanja 11 vya ndege ambavyo baadhi yake ukarabati na ujenzi wake umekamilika ama upo katika hatua za mwisho.

SEKTA YA BANDARI

Msigwa alisema, BandariSerikali inaendelea ya kazi za uboreshaji bandari zilizopo katika bahari, maziwa hasa kwa kutambua kuwa, bandari ni sehemu muhimu ya kimkakati katika uchumi wa nchi.

Alisema bahari na maziwa yaliyopo Tanzania yanategemewa na nchi zaidi ya nane kuanzia Bandari ya Dar es Salaam.

Uwekezaji mkubwa unaofanywa katika bandari hizo unaendelea kuongeza ufanisi ambapo katika kipindi cha kuanzia Oktoba-Desemba, 2022, idadi ya meli ambazo zinahuhudiwa na TPA katika Bandari za Bahari Kuu, Mwambao ilifikia meli 555.

Kati ya meli hizo, 308 zilikua za Bahari Kuu, 247 za mwambao sawa na ongezeko la asilimia 9 ya meli 510 zilizohudumiwa robo ya kwanza (Julai-Septemba, 2022).

Msigwa alisema, ongezeko hili ni sawa ma asilimia 16 ya meli 479 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita (Oktoba-Desemba 2021).

Pia kuanzia Oktoba-Desemba 2022, kiwango cha shehena kilichohudumiwa ni tani 6,333,115 sawa na asilimia 17.2, zaidi ya lengo la kuhudumia tani 5,403,609.

Shehena iliyohudumiwa ni zaidi ya asilimia 27 kwa shehena iliyohudumiwa kipindi kama cha Oktoba hadi Desemba, 2021 kikiwa tani 4,993,366. 

Bandari Kuu ya Dar es salaam ilihudumia tani 5,453,539 sawa na asilimia 86.1 ya mzigo wote uliyohudumiwa na TPA.

Upande wa makasha (Makontena) idadi ya makasha yaliyohudumiwa Oktoba-Desemba 2022 ilifikia (TEUs) 230,229 ambayo ni asilimia 12 zaidi ya lengo la kuhudumia makasha (TEUs) 203,850.

Makasha yaliyohudumiwa ni ongezeko la asilimia 22 ya makasha 188,838 yaliyohudumiwa katika kama hicho  Oktoba hadi Desemba 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *