Miamba 6 yatangulia AFCON 2025

Na Mwandishi Wetu

MIAMBA sita ya soka barani Afrika, imejikatia tiketi mapema za kufuzu kwa fainali za AFCON 2025 zitakazofanyikia nchini Morocco.

Nchi hizo ni Senegal, Angola, DR Congo, Misri, Burkina Faso na Cameroon ambazo zimefuzu huku kukiwa kumebaki mechi mbili kumaliza hatua ya makundi.

Katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia jana jijini hapa, wenyeji Senegal ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Malawi bao 1-0, likifungwa na nyota wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa anakipiga Al Nassr, Sadio Mane dakika za jioni.

Katika mchezo wa awali uliopigwa jijini Lilongwe, timu hizo zilitoka suluhu hivyo.

Ushindi huo, umeifanya Senegal kufikisha alama 10 kutoka Kundi L pamoja na Burkina Faso wakiwa tayari kwa fainali hizo.

Timu hiyo imefuzu licha ya kwamba mapema mwezi huu iliachana na Kocha wao wa muda mrefu,  

Aliou Cisse.

Burkina Faso ndio ilikuwa timu ya kwanza kufuzu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Burundi Jumapili.

Mabao yao yalifungwa na Mohamed Konate kwa mkwaju wa penalty kabla ya nyota wa zamani wa Aston Villa ambaye kwa sasa anakipiga Ajax, Bertrand Traore, kufunga bao la pili.

Kwa upande wa Cameroon, imefuzu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 jijini Kampala, Uganda mbele ya Kenya.

Ushindi huo umeifanya Cameroon kufikisha alama 10 Kundi J na imejihakikishia kumaliza nafasi ya pili mbele ya Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *