Samia awapiga ‘stop’ Mawaziri

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Mawaziri kuacha kuajiri Maafisa Habari binafsi badala yake wavitumie vitengo vya habari kutoa taarifa za Serikali.

Amezitaka Wizara kujibu kauli za upotoshaji ambazo zinatolewa na wanasiasa kuhusu utendaji wa Serikali.

Rais Dkt. Samia aliyasema hayo jana katika hotuba yake kwenye mkutano wa faragha unaoshirikisha Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu unaoendelea mkoani Arusha.

Rais Samia ameyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa Faragha (Retreat) ulioshirikisha Mawaziri, Makatibu Wakuu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC), jijini Arusha.

Lengo la mkutano huo ni ambao unafanyika kwa mara ya kwanza tangu Rais Samia aingie madarakani ni kuwakumbusha viongozi dhana ya uongozi, sifa za

kiongozi bora na utaratibu wa utoaji maamuzi ya kisera ndani ya Serikali.

Agizo hilo linatokana na kile alichokitolea mfano kuwa, amewahi kuibuka mwanasiasa aliyeikosoa Serikali akidai inatumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji, ilhali kuna visima kadhaa vilishachimbwa.

Alisema Wizara inayohusika na hilo ilipaswa kusimama haraka na kutoa ufafanuzi wa madai hayo badala ya kusubiri taarifa za upotoshaji zisambae.

“Nimewahi kuona kiongozi wa kisiasa akiilaumu Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji kupeleka kwa wananchi ilhali kuna visima kadhaa vilichimbwa nyuma na serikali iliviacha.

“Wizara inayohusika na hili ilipaswa kusimama haraka kujibu kutoa facts (ukweli), takwimu na kueleza kwanini visima hivyo viliachwa au havikuachwa,” alisema.

Rais Samia alifafanua kuwa, visima vilivyotajwa na mwanasiasa huyo ndiyo vilivyoisaidia Dar es Salaam wakati wa changamoto ya ukame.

“Najua kila Wizara ina kitengo cha habari, vitengo hivi vinatumikaje, vipo tu vimekaa havifanyi kazi lakini bado Mawaziri mmeajiri maafisa habari wenu binafsi wa kutoa taarifa zenu si taarifa za Serikali, hili tukarekebishe,” alisisitiza Rais Samia.

Alisema upo umuhimu mkubwa wa kuisemea serikali, viongozi wamekuwa wazito kuyasemea mafanikio mengi ya serikali hivyo kuacha watu wengine waendelee kufanya upotoshaji.

“Serikali imefanya mambo mengi yanayoondoa shida za wananchi hivyo ni wajibu wa viongozi kutoa taarifa za namna serikali ilivyotatua shida hizo,” aliongeza.

Rais Samia alisema, ili kujenga dhana ya uongozi bora, serikali imeandaa kikao hicho ili kuweka mstakabali wa mahusiano mazuri ya kulitumikia taifa.

Aliongeza kuwa, mada zitakazowasilishwa zitawafanya wateule hao wajitathmini kama wanaendana na misingi ya usimamizi bora wa rasilimali watu, fedha na mali zingine za serikali katika Wizara, mashirika wanayoyasimamia.

“Kutofanyika mikutano kama hii muda mrefu kumeleta athari zinazoonekana katika utendaji serikalini,” alisema.

Alisema umbwe la uelewa wa taratibu za utendaji kazi serikalini ni moja kati ya athati hizo hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima miongoni mwao, kuathiri utendaji kazi wao, uwezo wa kuhudumia wananchi.

Rais Dkt Samia alieleza moja ya sababu ya viongozi kubadilishwa mara kwa mara ni kuiepusha serikali na fedheha ya kuwa na viongozi wanaozifanya Wizara sehemu ya malumbano, migawanyiko isiyo na tija.

“Nafahamu madhara ya kubadilisha viongozi mara kwa mara, huwa sipendi kufanya hivyo kwa sababu kunafanya watu wafanye kazi kwa hofu, viongozi wasiwe na mipango ya muda mrefu kwa kuhofia teuzi zao kutenguliwa,” alisema.

Alisema kiongozi anapotolewa kazini inaleta fedheha kwa familia, watoto, vijana waliokuwa wanamuona mfano.

“Mimi si lengo langu kubadilisha viongozi mara kwa mara maana huchukua muda mrefu kuwajenga, wakati mwingine nalazimika kufanya hivyo ili kuepusha madhara zaidi kwa serikali na wananchi.

“Mkutano huu utawaongezea ujuzi katika uongozi na kuboresha utendaji wenu, ufanisi, kuondoa migongano mnapotoa huduma kwa wananchi.

“Tumeacha kazi nyingi tumejifungia Arusha kwa ajili hiyo, natarajia wote mtashiriki mkutano huu kikamilifu, sitofurahi kuona mtu mmoja anauchukulia mkutano huu kama sehemu ya kuwalenga viongozi wapya,” aliongeza.

Alifafanua kuwa mkutano huo ni muhimu zaidi kwa viongozi wazoefu ambao wanafanya kazi kwa mazoea, kuishi kwa migogoro na kutofuata taratibu.

“Viongozi wazoefu ndiyo wanaowafanya viongozi wapya wawaige wakiamini kutokufuata sheria na taratibu ni jambo la kawaida serikalini.

“Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara kuwa ninyi ni timu moja ya uongozi, utawala, mnategemewa kuonesha  njia ya nini kifanyike katika kutekeleza majukumu ya Wizara mlizokabidhiwa kuziongoza kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo na taratibu za serikali,” alieleza.

Alisema katika jukumu lao la utawala wanategemewa kuwa makini na mahiri, kusimamia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma.

Ili kukamilisha wajibu wao, hawana budi kutambua mipaka yao ya uongozi na mamlaka kwa kusoma miongozo ya utendaji kazi wao.

Rais Samia alisema ni wajibu wao kuzifahamu kwa kina shughuli za Wizara zao ili zifanyike kwa umakini, weledi kwani bila hivyo watashindwa kupanga majukumu, kuwasimamia walio chini yao.

Akizungumzia mada inayohusu utulivu na usalama wa nchi, alisema itawakumbusha kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya maadui wa ndani na nje.

Aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi hasa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

“Maendeleo makubwa na ya haraka yanapatikana kwa kufanya kazi na sekta binafsi za ndani na za kimataifa,  lazima viongozi tuhakikisha ofisi tunazoziongoza zinakuwa wezeshi badala ya kuwa vikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji,” aliongeza.

Alisema kila mmoja ahakikishe anavutia ustawi wa sekta binafsi nchini, kuepuka kauli zinazowafanya wawekezaji kutilia shaka dhamira ya serikali.

“Tunapokwenda nje tunakuwa na lugha nzuri tukiwaambia kuna hiki njooni muwekeze, wanapofika ofisini maneno wanayopewa yanawarudisha nyuma,” alisema Rais Samia.   

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *