Samatta arejea Stars kuivaa DR Congo

Na Badrudin Yahaya

NAHODHA wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, amerejea kwenye kikosi ikiwa ni maandalizi kuelekea mechi mbili za Kundi H kuwania tiketi ya michuano ya Afcon 2025 dhidi ya DR Congo.

Stars itakuwa ugenini Oktoba 10 kucheza dhidi ya DR Congo kabla ya miamba hao kurudiana tena Oktoba 15 katika mechi ambayo itachezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Samatta ambaye kwasasa anacheza PAOK FC ya Ugiriki, hakujumuishwa katika mechi za hivi karibuni za kikosi cha Stars na mara yake ya mwisho kuvaa jezi za timu hiyo ilikuwa ni Januari, mwaka huu wakati wa mchezo wa makundi wa michuano ya Afcon dhidi ya DR Congo.

Mbali na Samatta lakini Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amewaita kikosini nyota kadhaa kwa mara ya kwanza akiwemo mlinzi wa kati wa Simba, Abdulrazaq Hamza.

Nyota wengine walioingia ni Kipa wa Azam, Zuber Foba, Habib Khalid (Singida Black Stars), Seleman Mwalimu ‘Gomez’ (Fountain Gate), Nassor Saadun (Azam) na Abdullah Said (KMC).

Baadhi ya nyota ambao sio wageni katika kikosi hicho lakini hawakuwepo kwenye mchezo uliopita ni Kibu Denis (Simba) na Haji Mnoga.

Kocha Morocco katika kikosi hicho amewaacha nyota Abuutwalib Mshery na Nickson Kibabage (wote Yanga), huku pia jina la Simon Msuva likiendelea kuwa halipo kwa mara ya pili mfululizo katika vikosi vya hivi karibuni.

Timu hiyo inatarajia kuanza kuingia kambini mapema wiki hii kabla ya kuanza safari ya kwenda DR Congo mapema wiki ijayo.

Katika msimamo wa Kundi H, Stars ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 4 nyuma ya vinara DC Congo ambao wana alama sita baada ya kushinda mechi zao zote mbili za awali. Timu ya Ethiopia inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 1 na Guinea wanaburuza mkia wakiwa hawana kitu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *