Nyota 5 waliofanya mapinduzi Simba

Na Badrudin Yahaya

ILIKUWA sio rahisi kuweza kutabiri ni kipi kinaweza kutokea katika msimu huu kwa kikosi cha Simba SC ambacho kwa asilimia kubwa kimekusanya nyota wapya, lakini waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi.

Naam! Huu ni msemo tu kama ilivyokuwa misemo mingine lakini kwa upande wa Simba ni kweli nyota njema imeanza kuonekana.

Mechi tatu za msimu wa Ligi ya Tanzania Bara, wamekusanya alama tisa, mabao ya kufunga tisa, na hawajaruhusu bao lolote hii inakupa matumaini mema hasa kwa timu ambayo msimu uliopita ilionekana kuwa hovyo zaidi.

Sio tu kwenye ligi, hata katika mechi zao mbili za michuano ya Shirikisho Afrika ambazo wamecheza dhidi ya Al-Ahly Tripol ya Libya, kikosi cha Simba kimeonesha utayari wake wa kushindani mataji msimu huu.

Baada ya kuwa kwenye kivuli cha watani zao wajadi Yanga kwa misimu mitatu mfululizo, hii ni mara ya kwanza msimu huu Simba wanaonekana kupania kwenda jino kwa jino.

Chini ya Kocha mpya, Fadlu Davids, kikosi hicho kinaonesha uimara wake kila kukicha lakini kubwa zaidi kiwango chao kinaonekana kuegemea kwa nyota kadhaa wapya ambao wamesajiliwa msimu huu.

Deborah Fernandez

Wakati anasajiliwa uliibuka mzaha mkubwa hasa kuhusu jina lake lakini pia timu aliyotoka ya Mutondo Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Zambia.

Wengi waliamini mchezaji huyo wa kiungo (box to box) asingeweza kufanya vizuri kwenye Ligi ya Tanzania kwakuwa alitoka katika timu ambayo haikuwa ikifanya vizuri nchini Zambia.

Hata hivyo Deborah mchezaji mwenye uraia wa Angola na DR Congo ameibuka kuwa moja kati ya nyota wa kutumainiwa zaidi kwenye kikosi cha Simba chini ya Fadlu.

Moussa Camara

Usajili wake ulikuja baada ya kuumia kwa kipa namba moja, Ayoub Lakred wakati timu ilipokuwa Misri kwenye maandalizi ya msimu mpya.

Katika mipango ya Simba hakukuwa na dalili ya kusajili kipa mpya tofauti na waliokuwepo awali ambao walimaliza msimu lakini kuumia kwa Ayoub kuliifanya timu hiyo kwenda kupata kipa halisi ambaye anaweza kuwavusha katika hatua kubwa.

Alisajiliwa akitokea kwenye kikosi cha Horoya ya nchini kwao Guinea na sasa ameingia kwenye vichwa vya habari akionekana kuwa ni mshindani halisi wa Djigui Diarra wa Yanga ambaye ametamba kwa miaka mitatu mfululizo.

Abdulrazaq Hamza

Usajili wake ulichukuliwa kama usajili wakawaida hasa ukizingatia kuwa ni mchezaji mzawa.

Baada ya kuondoka Henock Inonga, watu wengi walitegemea kuona pengo lake lingezibwa na beki mwengine wa kimataifa.

Ujio wa Chamou Karabou raia wa Ivory Coast uliwafanya watu wengi kuamini kuwa huyo ndiye atakayezima katikati ya eneo la ulinzi na Che Malone Fondoh.

Hata hivyo jina la Hamza limekuwa likitajwa kusimama kati na Malone na siku hadi siku watu wameshaanza kuelewa uwezo halisi wa mchezaji huyo.

Hakuwahi kuwa maarufu katika soka la ndani lakini mchezaji huyo aliwahi kupita katika timu ya vijana ya Azam kisha akacheza Mbeya City kabla hajapaa kwenda Afrika Kusini ambapo alijiunga na Super Sport.

Jean Charles Ahoua

Licha ya kupewa majukumu makubwa ya kuziba pengo la Saido Ntibanzokiza na Clatous Chama lakini watu wengi hawakuwa na Imani naye.

Kilichokuwa kinawatisha watu wengi ni kwasababu Jean Charles Ahoua licha ya kutokea Ivory Coast lakini hajacheza timu kubwa za pale mfano Asec Mimos.

Yeye ametokea Stella Club lakini akiwa na timu hiyo alifanikiwa kuwa MVP wa msimu wa 2023-24 baada ya kufunga mabao 9 na kutengeneza 12.

Tangu amejiunga Simba taratibu ameanza kuonesha umwamba wake ambapo katika mechi za ligi kuu tatu alizocheza tayari ametengeneza mabao manne na kufunga moja.

Leonel Ateba

Simba walishaamua kufunga hesabu zao katika usajili kabla ya kocha Fadlu kuwaambia kuwa anataka nyota mwengine katika eneo la ushambuliaji.

Leonel Ateba raia wa Cameroon aliingi Simba siku ya mwisho kabisa ya dirisha la usajili na hiyo ilimfanya kushindwa kucheza mechi mbili za mwanzo za ligi kuu.

Hata hivyo kazi yake ilianza kuonekana kwenye mechi za kimataifa na kisha moto wake akauhamishia katika Ligi kuu ya Tanzania ambapo mechi yake ya kwanza alifunga bao dhidi ya Azam.

Kwaenye mechi yake ya kwanza tu ndani ya Ligi kiwango chake kinaonesha kuwavuta wengi na anatarajia kuwa mmoja kati ya nguzo kwenye msimu wa Simba wa Ubaya Ubwela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *